Mapigo Saba ya Mwisho
Wale waliomkataa yule mnyama wanasimama kando ya bahari ya kioo wakiimba wimbo wa Musa na wa Mwana-Kondoo, wakiziita njia za Baba yetu kuwa za haki na za kweli. Malaika saba wanatoka wamevaa kitani king'aacho wakiwa na mabakuli saba, na moshi unalijaza hekalu hata hakuna awezaye kuingia mpaka yamiminwe.
15 1Nikaona ishara nyingine mbinguni, kuu na ya ajabu: malaika saba wakiwa na mapigo saba ya mwisho, kwa maana katika hayo ghadhabu ya Baba yetu ilikamilika.
2Nikaona kitu kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyika na moto, na wamesimama kando yake wale walioushinda mnyama, na sanamu yake, na tarakimu ya jina lake, wakiwa na vinubi kutoka kwa Baba yetu. 3Nao waliimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Baba yetu, na wimbo wa Yesu, Mwana-Kondoo: "Kuu na ya ajabu ni matendo yako, Ee Baba, Bwana Mwenyezi! Za haki na za kweli ni njia zako, Mfalme wa mataifa! 4Ni nani asiyekuogopa wewe, Ee Baba, na kulitukuza jina lako? Kwa maana wewe peke yako ndiwe mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kuabudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamefunuliwa."
5Baada ya hayo nikatazama, na hekalu la hema ya ushuhuda likafunguliwa mbinguni. 6Wale malaika saba wenye mapigo saba wakatoka hekaluni, wamevaa kitani safi king'aacho, na mikanda ya dhahabu vifuani mwao.
7Kisha mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Baba yetu, aliye hai milele na milele. 8Nao moshi kutoka kwa utukufu wa Baba yetu na kutoka kwa nguvu zake ukalijaza hekalu; wala hakuna aliyeweza kuingia ndani yake mpaka yatakapokamilika mapigo saba ya wale malaika saba.