Mwanangu, Nipe Moyo Wako
Adabu za mezani zenye jambo zito zaidi chini yake. Jihadhari mbele ya vyakula vitamu vya mtawala, wala usijitaabishe ukikimbiza utajiri unaoota mabawa na kuruka. Inaishia kwa picha ya mlevi, akipigwa bila kuhisi, akiamka ili tu kutafuta kinywaji kingine.
23 1Uketipo kula chakula pamoja na mtawala, angalia kwa makini kilicho mbele yako, 2na uweke kisu kooni mwako ikiwa wewe ni mtu utawaliwaye na tamaa. 3Usitamani vyakula vyake vitamu, kwa maana ni chakula cha udanganyifu.
4Usijitaabishe ili kupata utajiri; uwe na hekima ya kujizuia. 5Mara utazamapo utajiri, umetoweka, kwa maana ghafula huota mabawa na kuruka kuelekea mbinguni kama tai.
6Usile mkate wa mtu bahili, wala usitamani vyakula vyake vitamu, 7kwa maana yeye ni mtu wa aina ile anayeendelea kuhesabu gharama. "Kula na kunywa!" akuambia, lakini moyo wake hauko pamoja nawe. 8Utakitapika kile kidogo ulichokula, nawe utakuwa umepoteza maneno yako ya kupendeza.
9Usiseme masikioni mwa mpumbavu, kwa maana atadharau hekima ya maneno yako.
10Usisogeze jiwe la mpaka la zamani, wala usiingilie mashamba ya yatima, 11kwa maana Mkombozi wao ana nguvu; Baba yetu atatetea shauri lao dhidi yako. a a v11 Mtu amkoseapo yatima asiye na mtu wa kumtetea, Baba yetu mwenyewe huwa mtetezi wao na hulichukua shauri lao kuwa lake mwenyewe.
12Elekeza moyo wako kwenye mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
13Usimzuilie mtoto adhabu; ukimpiga kwa fimbo, hatakufa. 14Mpige kwa fimbo, nawe utaiokoa nafsi yake kutoka kaburini.
15Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu nao utafurahi. 16Utu wangu wa ndani utashangilia midomo yako inenapo yaliyo sawa.
17Usiuache moyo wako uwaonee wivu wenye dhambi, bali udumu katika kumcha Baba yetu mchana kutwa. 18Hakika kuna siku zijazo, na tumaini lako halitakatiliwa mbali.
19Sikia, mwanangu, uwe na hekima, na uuweke moyo wako katika njia iliyo sawa. 20Usiwe miongoni mwa walevi wa mvinyo au wale wajishibishao nyama, 21kwa maana mlevi na mlafi watakuja kuwa maskini, na usingizi utawavika matambara.
22Msikilize baba yako aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee. 23Nunua kweli wala usiiuze; nunua hekima, mafundisho, na ufahamu. 24Baba wa mtoto mwenye haki atafurahi sana; yeye amzaaye mwana mwenye hekima atapata furaha kwake. 25Baba yako na mama yako na wafurahi; yeye aliyekuzaa na ashangilie.
26Mwanangu, nipe moyo wako, na macho yako yafurahie njia zangu. 27Kwa maana kahaba ni shimo refu, na mwanamke mzinzi ni kisima chembamba. 28Yeye huvizia kama mnyang'anyi na huwaongoza wanaume wengi katika ukosefu wa uaminifu.
29Ni nani mwenye taabu? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani mwenye majeraha bila sababu? Ni nani mwenye macho mekundu? 30Ni wale wakaao muda mrefu kwenye mvinyo, wale waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa. 31Usiukazie macho mvinyo ungali mwekundu, ungali unang'aa kikombeni na kushuka taratibu. 32Mwishoni huuma kama nyoka na huchoma kama fira. 33Macho yako yataona mambo ya ajabu, na moyo wako utanena mambo yaliyopotoka. 34Utakuwa kama mtu alalaye katikati ya bahari, kama mtu alalaye juu ya mlingoti wa merikebu. 35"Walinipiga, lakini sikuumia; walinicharaza, lakini sikujua. Nitaamka lini? Nitatafuta kinywaji kingine."