Hekima Hujenga Nyumba
Kujenga na kuokoa. Nyumba hujengwa kwa hekima, na mwenye haki huanguka mara saba na kuinuka tena. Inakataa furaha ya kuanguka kwa adui, na inakataa udhuru wa kusema hatukujua watu wanapochukuliwa kwenda kufa. Shamba la mizabibu lililosongwa na magugu ndilo linalofundisha hilo.
24 1Usiwaonee wivu watu waovu, wala usitamani kuwa pamoja nao, 2kwa maana mioyo yao hupanga jeuri, na midomo yao hunena maneno ya taabu.
3Kwa hekima nyumba hujengwa, na kwa ufahamu huimarishwa; 4na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa mali zote za thamani na za kupendeza.
5Mtu mwenye hekima amejaa nguvu, na mtu mwenye maarifa huzidisha uwezo wake, 6kwa maana kwa mwongozo wa hekima waweza kupigana vita vyako, na ushindi huja kwa washauri wengi.
7Hekima i juu mno kwa mpumbavu; langoni, hana lolote la kusema. 8Kila apangaye kutenda mabaya ataitwa mwenye hila. 9Hila za mpumbavu ni dhambi, na mwenye dharau ni chukizo kwa watu.
10Ukilegea siku ya taabu, nguvu zako ni ndogo. 11Waokoe wale wanaochukuliwa kwenda kufa, na uwazuie wale wanaojikwaa kuelekea kuchinjwa. 12Ukisema, "Tazama, hatukujua jambo hili," je, yeye apimaye mioyo hataliona? Je, yeye ailindaye nafsi yako hatalijua? Naye je, hatamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake?
13Mwanangu, kula asali, kwa maana ni njema, na matone ya sega ni matamu kinywani mwako. 14Ujue kwamba hekima ni hivyo kwa nafsi yako; ukiipata, kuna wakati ujao, na tumaini lako halitakatiliwa mbali.
15Usiotee, ewe mtu mwovu, dhidi ya makao ya mwenye haki; usipaharibu mahali pake pa kupumzika, 16kwa maana ijapokuwa mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena, bali waovu hujikwaa katika msiba.
17Usifurahi adui yako aangukapo, wala moyo wako usishangilie ajikwaapo, 18Baba yetu asije akaliona, likamchukiza, akaugeuza mbali hasira yake naye.
19Usisumbuke moyo kwa sababu ya watenda maovu, wala usiwaonee wivu waovu, 20kwa maana mtu mwovu hana wakati ujao; taa ya waovu itazimwa.
21Mwanangu, mche Baba yetu na mfalme, wala usiungane na wale wanaowaasi, 22kwa maana msiba wao utainuka ghafula, naye ni nani ajuaye uharibifu ambao wote wawili waweza kuleta?
Haki Bila Upendeleo
23Haya nayo ni maneno ya wenye hekima: Kuonyesha upendeleo katika hukumu si vyema. 24Yeye amwambiaye mwenye hatia, "Wewe huna hatia," mataifa watamlaani na watu watamkemea, 25bali itakuwa heri kwa wale wamhukumuo mwenye hatia, na baraka tele itawajilia. 26Jibu la unyofu ni kama busu la midomoni. 27Tengeneza kazi yako ya nje, andaa mashamba yako, na baada ya hayo jenga nyumba yako. 28Usiwe shahidi dhidi ya jirani yako bila sababu; je, utadanganya kwa midomo yako? 29Usiseme, "Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; nitamlipa mtu huyo kwa aliyoyatenda." 30Nilipita karibu na shamba la mtu mvivu, karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili, 31na tazama, lote lilikuwa limemea miiba; ardhi ilifunikwa na magugu, na ukuta wake wa mawe ulikuwa umebomoka. 32Ndipo nikatazama nikatia moyoni; nikaona nikapokea mafundisho. 33Bado usingizi kidogo, kusinzia kidogo, kukunja mikono kidogo ili kupumzika, 34ndipo umaskini utakujilia kama mnyang'anyi, na uhitaji kama mtu mwenye silaha.