Mkusanyo wa Hezekia
Zilinakiliwa na watu wa Hezekia, nazo zimejaa mifano kwa njia isiyo ya kawaida: matofaa ya dhahabu, theluji wakati wa mavuno, jino bovu, siki juu ya magadi, mji usio na kuta. Mashauri yake ni ya wazi kabisa, kuanzia kutojitukuza mbele ya mfalme hadi kutomchosha jirani yako kwa kwenda kwake mara kwa mara.
25 1Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia mfalme wa Yuda waliziandika. 2Ni utukufu wa Baba yetu kuficha jambo, bali ni utukufu wa wafalme kulichunguza jambo. 3Kama mbingu zilivyo juu na dunia ilivyo na kina, ndivyo mioyo ya wafalme isivyochunguzika. 4Ondoa takataka katika fedha, na chombo hutokea kwa msonga vyuma. 5Ondoa waovu mbele ya mfalme, na kiti chake cha enzi kitaimarishwa katika haki. 6Usijitukuze mbele ya mfalme, wala usisimame mahali pa wakuu; 7kwa maana ni afadhali kuambiwa, "Panda hapa juu," kuliko kushushwa mahali pa chini mbele ya mtukufu unayemwona. 8Usifanye haraka kuingia kwenye ugomvi, kwa maana utafanya nini mwishoni jirani yako atakapokuaibisha? 9Toa hoja yako na jirani yako mwenyewe, lakini usifunue siri ya mwingine, 10asije yeye aisikiaye akakuaibisha, na sifa yako mbaya isiondoke kamwe. 11Neno linalonenwa wakati ufaao ni kama matofaa ya dhahabu katika vyombo vya fedha. 12Kama pete ya dhahabu au pambo la dhahabu safi ndivyo lilivyo karipio la hekima kwa sikio lisikiazo. 13Kama ubaridi wa theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao; huiburudisha nafsi za bwana zake. 14Kama mawingu na upepo pasipo mvua ndivyo alivyo yule ajisifiaye kwa zawadi asiyoitoa kamwe. 15Kwa uvumilivu mtawala hushawishiwa, na ulimi laini huvunja mfupa. 16Ukiona asali, kula kiasi tu, usije ukaila kupita kiasi ukatapika. 17Usiende nyumbani kwa jirani yako mara kwa mara, asije akakuchoka na kukuchukia. 18Kama rungu, na upanga, na mshale mkali ndivyo alivyo mtu ashuhudiaye uongo dhidi ya jirani yake. 19Kama jino bovu au mguu uliotoka katika kiungo ndivyo ulivyo utegemezi kwa mtu asiye mwaminifu wakati wa taabu. 20Kama yule avuaye vazi siku ya baridi, kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yule amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito. 21Adui yako akiwa na njaa, mpe mkate ale, na akiwa na kiu, mpe maji anywe; 22kwa maana utamrundikia makaa ya moto juu ya kichwa chake, na Baba yetu atakupa thawabu. 23Upepo wa kaskazini huleta mvua, na ulimi wa siri, nyuso zenye hasira. 24Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini kuliko kukaa nyumba moja na mke mgomvi. 25Kama maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali. 26Kama chemchemi iliyotibuliwa au kisima kilichochafuliwa ndivyo alivyo mwenye haki ashindwaye mbele ya waovu. 27Si vyema kula asali kupita kiasi, wala kutafuta utukufu wako mwenyewe. 28Kama mji uliobomolewa na kuachwa bila kuta ndivyo alivyo mtu asiyeweza kuitawala roho yake mwenyewe.