Mpumbavu Hurudia Upumbavu Wake
Karibu ni orodha ya aina tatu za watu. Mpumbavu, asiyeweza kuheshimiwa wala kuajiriwa wala kuponywa; mvivu, ageukaye kitandani mwake kama mlango katika bawaba zake; na mdanganyifu, ajeruhiye kisha akasema alikuwa akicheza tu. Achimbaye shimo huanguka ndani yake.
26 1Kama theluji wakati wa kiangazi na kama mvua wakati wa mavuno, ndivyo heshima isivyomstahili mpumbavu. 2Kama shomoro apapurikaye au mbayuwayu arukaye kwa haraka, ndivyo laana isiyostahili isivyotua. 3Mjeledi kwa farasi, hatamu kwa punda, na fimbo kwa migongo ya wapumbavu. 4Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake, usije ukafanana naye wewe mwenyewe. 5Mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake, asije akawa na hekima machoni pake mwenyewe. 6Atumaye ujumbe kwa mkono wa mpumbavu hujikata miguu yake mwenyewe na kunywa jeuri. 7Kama miguu ya kilema iangikavyo bila faida, ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha wapumbavu. 8Kama afungaye jiwe katika kombeo, ndivyo alivyo ampaye heshima mpumbavu. 9Kama mwiba ulivyo katika mkono wa mlevi, ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha wapumbavu. 10Kama mpiga upinde ajeruhiye kila mtu, ndivyo alivyo amwajiriye mpumbavu au amwajiriye kila apitaye. 11Kama mbwa arudiavyo kwenye matapiko yake, ndivyo mpumbavu arudiavyo upumbavu wake. 12Je, wamwona mtu mwenye hekima machoni pake mwenyewe? Kuna tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake yeye.
13Mvivu husema, "Kuna simba njiani! Simba yuko barabarani!" 14Kama mlango ugeukavyo katika bawaba zake, ndivyo mvivu ageukavyo kitandani mwake. 15Mvivu huutumbukiza mkono wake sahanini; humchosha kuurudisha kinywani mwake. 16Mvivu ana hekima zaidi machoni pake mwenyewe kuliko watu saba wajibuo kwa busara.
17Kama amkamataye mbwa masikio, ndivyo alivyo apitaye ajiingizaye katika ugomvi usiokuwa wake.
18Kama mwendawazimu arushaye vinga vya moto, mishale, na mauti, 19ndivyo alivyo yule amdanganyaye jirani yake na kusema, "Nilikuwa nikicheza tu!"
20Bila kuni moto huzimika, na bila mchongezi ugomvi hutulia. 21Kama makaa yalivyo kwa kaa la moto na kuni kwa moto, ndivyo alivyo mtu mgomvi awashaye ugomvi. 22Maneno ya mchongezi ni kama chembe tamu; hushuka mpaka pande za ndani za tumbo.
23Kama rangi ing'aayo ifunikavyo chungu cha udongo, ndivyo yalivyo midomo laini yenye moyo mbaya. 24Adui hujigeuza kwa midomo yake, lakini moyoni mwake huficha hila. 25Anenapo kwa neema, usimwamini, kwa maana machukizo saba yamejaa moyoni mwake. 26Ingawa chuki yake imefichwa kwa hila, uovu wake utafichuliwa katika kusanyiko. 27Achimbaye shimo atatumbukia ndani yake, na jiwe humrudia yule alivingirishaye. 28Ulimi wa uongo huwachukia wale uwapondao, na kinywa cha kujipendekeza huleta uharibifu.