Kuwaombea Watu Wote
Paulo anaomba kwanza kwamba maombi yafanywe kwa ajili ya watu wote, wafalme pia, kwa kuwa Baba yetu anataka watu wote waokolewe, na mpatanishi mmoja, Kristo Yesu, alijitoa kwa ajili ya wote. Kisha wanaume waombe pasipo hasira, na wanawake wavae kwa kiasi, wajifunze kwa utulivu, wala wasifundishe.
2 1Basi, kwanza kabisa, nasihi maombi, na sala, na dua, na shukrani zitolewe kwa ajili ya watu wote, 2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya amani na utulivu, katika utauwa wote na heshima. 3Jambo hili ni jema, nalo lampendeza Baba yetu, Mwokozi wetu, 4yeye atakaye watu wote waokolewe na kuufikia ujuzi wa kweli. 5Kwa maana Baba ni mmoja, na mpatanishi kati ya Baba na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu, 6aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wote—ushuhuda uliotolewa kwa wakati wake. 7Kwa ajili ya jambo hili naliwekwa kuwa mhubiri na mtume—nasema kweli, sisemi uongo—mwalimu wa mataifa katika imani na kweli. 8Napenda basi wanaume waombe kila mahali, wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala mashindano.
9Vivyo hivyo, wanawake najivike mavazi ya kujisitiri, wenye adabu na kiasi, si kwa kusuka nywele, wala dhahabu, wala lulu, wala mavazi ya thamani kubwa, 10bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kumcha Baba yetu. 11Mwanamke na ajifunze kwa utulivu, katika utii wote. 12Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume; bali akae kimya. 13Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, kisha Hawa. 14Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa akaingia katika kosa. 15Lakini ataokolewa kwa kuzaa watoto, wakidumu katika imani, na upendo, na utakatifu, pamoja na kiasi. a a v15 Kiwakilishi hubadilika kutoka 'yeye' kwenda 'wao' — kama ilivyo katika lugha ya asili — yaelekea kikiwarejelea wanawake kwa ujumla wanaodumu katika sifa hizi njema.