Macho Yamekazwa Kwako
Zaburi ya Daudi.
141 1 Baba yangu, ninakuita; njoo haraka kwangu. Sikiliza sauti yangu ninapokulilia.
2 Maombi yangu na yapande mbele zako kama uvumba, kuinuliwa kwa mikono yangu kuwe kama sadaka ya jioni.
3 Weka mlinzi, Baba yangu, juu ya kinywa changu; ulinde mlango wa midomo yangu. 4 Usiuache moyo wangu ugeukie uovu wowote, kushiriki matendo maovu pamoja na watendao mabaya; wala usiniache nile vyakula vyao vitamu.
5 Mwenye haki na anipige —ni fadhili; na anirekebishe—ni mafuta kichwani mwangu; kichwa changu hakitakataa. Lakini maombi yangu daima ni kinyume cha matendo ya waovu.
6 Watawala wao watakapotupwa chini kutoka majabali, ndipo watu watakaposikia maneno yangu, kwa maana ni matamu. 7 Kama mtu alimavyo na kupasua ardhi, ndivyo mifupa yetu ilivyotawanyika kwenye mdomo wa kaburi.
8 Lakini macho yangu yamekazwa kwako, Baba yangu Mwenye enzi; kwako nakimbilia— usiniache bila kinga. 9 Niepushe na mtego walionitegea, na mitego ya watendao mabaya. 10 Waovu na waanguke katika nyavu zao wenyewe, hali mimi peke yangu napita salama.