Nilifungua, Naye Alikuwa Amekwenda
Anasema ameingia bustanini mwake. Kisha mwanamke anasimulia juu ya usiku ambao alisita mlangoni na kufungua kwa kuchelewa, akamkuta ameondoka. Alipokuwa akimtafuta, walinzi walimpiga. Alipoulizwa ni nini kinachomfanya awe wa tofauti, anamweleza kuanzia kichwani hadi miguuni.
5 1Nimeingia bustanini mwangu, dada yangu, bibi arusi wangu; nimekusanya manemane yangu pamoja na kiungo changu, nimekula sega langu la asali pamoja na asali yangu, nimekunywa divai yangu pamoja na maziwa yangu. Kuleni, enyi rafiki; kunyweni, tena kunyweni sana, enyi wapendanao!
2Nililala, lakini moyo wangu ulikuwa macho. Sauti—mpenzi wangu anabisha: "Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu, njiwa wangu, mkamilifu wangu, kwa maana kichwa changu kimelowa umande, nywele zangu kwa matone ya usiku." 3Nilikuwa nimevua vazi langu— nitalivaaje tena? Nilikuwa nimenawa miguu yangu— nitaichafuaje? 4Mpenzi wangu alitia mkono wake tunduni mwa komeo, na moyo wangu ukatetemeka ndani yangu. 5Niliinuka nimfungulie mpenzi wangu mlango, na mikono yangu ilidondosha manemane, vidole vyangu manemane yaliyoyeyuka, juu ya vishikizo vya komeo. 6Nilimfungulia mpenzi wangu mlango, lakini mpenzi wangu alikuwa amegeuka na kwenda zake. Nafsi yangu ilizimia aliponena. Nilimtafuta, lakini sikumwona; nilimwita, lakini hakunijibu. 7Walinzi walinikuta walipokuwa wakizunguka mjini; walinipiga, walinijeruhi; walininyang'anya joho langu, walinzi hao wa kuta. 8Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kama mkimwona mpenzi wangu, mwambieni kwamba ninaugua kwa mapenzi. 9Mpenzi wako ana ubora gani kuliko mpenzi mwingine, ewe mzuri kuliko wanawake wote? Mpenzi wako ana ubora gani kuliko mpenzi mwingine, hata ukatusihi hivi?
10Mpenzi wangu ang'aa na ni mwekundu, bora kuliko elfu kumi. 11Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote; nywele zake zimepindapinda, nyeusi kama kunguru. 12Macho yake ni kama njiwa kando ya vijito vya maji, yaliyooshwa kwa maziwa, yaliyowekwa kama vito mahali pake. 13Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo, minara ya mimea yenye harufu nzuri. Midomo yake ni yungiyungi, ikidondosha manemane yaliyoyeyuka. 14Mikono yake ni fito za dhahabu, iliyowekwa vito. Kiwiliwili chake ni pembe za ndovu zilizong'aa, zilizopambwa kwa yakuti samawi. 15Miguu yake ni nguzo za marmari, iliyosimikwa juu ya vitako vya dhahabu safi. Sura yake ni kama Lebanoni, bora kama mierezi. 16Kinywa chake ni utamu wenyewe, naye anatamanika kabisa. Huyu ndiye mpenzi wangu, na huyu ndiye rafiki yangu, enyi binti za Yerusalemu.