Ulimi wa Majivuno
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya hekima ya Daudi. Doegi Mwedomi alipokuja na kumwambia Sauli, "Daudi amefika nyumbani kwa Ahimeleki."
Imeelekezwa kwa Doegi, aliyewafichua makuhani kwa Sauli. Anasemeshwa kama mtu apendaye maneno ya kumeza-meza na anayetegemea mali yake mwenyewe, na anaambiwa atang'olewa katika hema lake — huku mwimbaji akistawi kama mzeituni nyumbani mwa Baba yetu.
52 1Kwa nini unajivunia ubaya, wewe uliye hodari? Upendo mwaminifu wa Baba yetu wadumu mchana kutwa.
2Ulimi wako wapanga uharibifu, kama wembe ulionolewa, wewe mdanganyifu. 3Unapenda ubaya kuliko wema, na uongo kuliko kunena yaliyo ya haki.
4Unapenda kila neno la kumeza-meza, wewe ulimi wa hila. 5Lakini Baba yetu atakubomoa milele; atakunyakua na kukung'oa katika hema lako; atakung'oa katika nchi ya walio hai.
6Wenye haki wataona na kuogopa; watamcheka, wakisema, 7"Mtazameni mtu ambaye hakumfanya Baba yetu kuwa kimbilio lake, bali alitegemea wingi wa mali yake na kupata nguvu kwa kuwaangamiza wengine." 8Bali mimi ni kama mzeituni ustawio nyumbani mwa Baba yetu; nautumaini upendo mwaminifu wa Baba yetu milele na milele. 9Nitakusifu milele kwa uliyoyatenda; mbele ya waaminifu wako nitaliweka tumaini langu katika jina lako, kwa maana ni jema.