Jinsi Ilivyo Vyema Kumwimbia Sifa
147 1 Haleluya! Jinsi ilivyo vyema kumwimbia sifa Baba yetu; jinsi kilivyo kupendeza na kufaa kumsifu.
2 Baba yetu anaijenga Yerusalemu; anawakusanya watu wa Israeli waliotawanyika. 3 Anawaponya waliovunjika moyo, na kuvifunga vidonda vyao. 4 Anazihesabu nyota; anaziita zote kwa majina yake. 5 Baba yetu Mtawala ni mkuu, na mwenye nguvu nyingi; ufahamu wake hauna kipimo. 6 Baba yetu anawainua wanyenyekevu; anawaangusha waovu chini ardhini.
7 Mwimbieni Baba yetu kwa shukrani; mpigieni muziki kwa kinubi. 8 Anazifunika mbingu kwa mawingu; anaipelekea nchi mvua; anayafanya majani kumea vilimani. 9 Anawapa wanyama chakula chao, na makinda ya kunguru yanapolia. 10 Furaha yake haiko katika nguvu za farasi, wala hapendezwi na miguu ya mwanadamu. 11 Moyo wa Baba yetu hufurahia wale wanaomcha yeye, wale wanaotumaini upendo wake wa agano.
12 Msifu Baba yetu, ee Yerusalemu! Msifu Baba yako, ee Sayuni! 13 Kwa maana anaimarisha makomeo ya malango yako; anawabariki watoto wako ndani ya kuta zako. 14 Analeta amani katika mipaka yako; anakushibisha kwa ngano iliyo bora. 15 Anaipeleka amri yake duniani; neno lake hupiga mbio kwa haraka. 16 Anatoa theluji kama sufu; anasambaza barafu kama majivu. 17 Anavurumisha mvua yake ya mawe kama makombo; ni nani awezaye kusimama mbele ya baridi yake? 18 Analituma neno lake na kuiyeyusha barafu; anauamsha upepo wake, na maji yanatiririka. 19 Analitangaza neno lake kwa Yakobo, sheria zake na hukumu zake kwa Israeli. 20 Hajalitenda hili kwa taifa lingine lolote; hawazijui hukumu zake. Haleluya!