Twendeni Nyumbani Kwake
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
Furaha ya msafiri wa hija anapofika nyumbani kwa Baba yetu, miguu yake hasa ikisimama ndani ya malango. Mji ndipo makabila yanapokutana na ambapo hukumu ya haki inatolewa, kwa hiyo anaiombea amani yake, na anasema anafanya hivyo kwa ajili ya ndugu zake, si kwa ajili yake mwenyewe.
122 1Nilifurahi pamoja na wale walioniambia, "Twendeni nyumbani kwa Baba yetu." 2Miguu yetu inasimama ndani ya malango yako, ee Yerusalemu. 3Yerusalemu, uliojengwa kama mji ulioshikamana pamoja imara, 4ambako makabila hupanda, makabila ya Baba yetu, kama amri kwa Israeli, ili kulishukuru jina la Baba yetu. 5Kwa maana huko viti vya enzi vya hukumu viliwekwa, viti vya enzi vya nyumba ya Daudi.
6Ombeni amani ya Yerusalemu: "Wapate raha wale wakupendao. 7Amani na iwe ndani ya kuta zako, salama ndani ya ngome zako." 8Kwa ajili ya ndugu zangu na wenzangu, nitasema, "Amani na iwe ndani yako." 9Kwa ajili ya nyumba ya Baba yetu nitautafuta wema wako.