Nuru ya Baba Haiwezi Kuzuiliwa
Kinara cha dhahabu kinacholishwa na mizeituni miwili kinajibu kukata tamaa kwa Zerubabeli juu ya hekalu dogo, ambalo halijakamilika. Neno la Baba yetu kwake: si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa Roho wangu. Mikono iliyoweka msingi ndiyo itakayoumaliza; wala mtu asidharau mambo madogo.
4 1Kisha yule malaika aliyesema nami akarudi, akaniamsha, kama mtu aamshwavyo usingizini. 2Akaniuliza, "Waona nini?" Nikasema, "Nimeona kinara cha taa cha dhahabu, na bakuli juu yake, na taa zake saba, na mifereji saba kwa kila taa iliyo juu yake.
3Na mizeituni miwili karibu nacho, mmoja upande wa kuume wa bakuli, na mwingine upande wake wa kushoto."
4Nikamjibu yule malaika aliyesema nami, nikasema, "Ni nini hivi, bwana wangu?"
5Ndipo yule malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, "Hujui hivi ni nini?" Nikasema, "La, bwana wangu."
6Akajibu, akaniambia, "Hili ndilo neno la Baba yetu kwa Zerubabeli, kusema: Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa Roho yangu, asema Baba wa majeshi ya mbinguni. 7Wewe ni nani, ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare. Naye ataleta jiwe la kilele, huku wakipiga kelele, wakisema, 'Neema, neema iwe juu yake!'"
8Tena neno la Baba yetu likanijia, kusema,
9"Mikono ya Zerubabeli imeuweka msingi wa nyumba hii; na mikono yake ndiyo itakayoumaliza. Nawe utajua ya kuwa Baba wa majeshi ya mbinguni amenituma kwenu. 10Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Watafurahi wakati watakapoliona timazi mkononi mwa Zerubabeli. Hizi saba ni macho ya Baba yetu, yatembeayo huku na huku duniani mwote."
11Ndipo nikamjibu, nikamwambia, "Ni nini hii mizeituni miwili, iliyo upande wa kuume na upande wa kushoto wa kinara?" 12Nikauliza mara ya pili, nikamwambia, "Ni nini matawi haya mawili ya mzeituni, yaliyo karibu na mirija miwili ya dhahabu, imwagayo mafuta ya dhahabu?"
13Akanijibu, akaniambia, "Hujui hivi ni nini?" Nikasema, "La, bwana wangu."
14Ndipo akasema, "Hawa ndio wale wawili waliotiwa mafuta, wasimamao mbele ya Bwana wa dunia yote."