Wimbo Mpya kwa Dunia Yote
96 1 Mwimbieni Baba yetu wimbo mpya; mwimbieni Baba yetu, dunia yote.
2 Mwimbieni Baba yetu, libarikini jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. 3 Hubirini matendo yake matukufu katika mataifa, kazi zake za ajabu miongoni mwa watu wote. 4 Kwa maana Baba yetu ni mkuu, mwenye kustahili sana kusifiwa; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. 5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, bali Baba yetu ndiye aliyeziumba mbingu. 6 Fahari na utukufu ziko mbele zake; nguvu na uzuri vimo patakatifu pake.
7 Mpeni Baba yetu, enyi jamaa zote za mataifa, mpeni Baba yetu utukufu na nguvu. 8 Mpeni Baba yetu utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka, mkaingie nyua zake. 9 Mwabuduni Baba yetu katika fahari ya utakatifu; tetemekeni mbele zake, dunia yote. 10 Semeni katika mataifa, "Baba yetu anatawala! Ulimwengu umethibitika, hautaondoshwa kamwe. Atawahukumu watu kwa haki."
11 Mbingu na zifurahi, na dunia ishangilie; bahari na ivume, na vyote viijazavyo. 12 Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo; ndipo miti yote ya msituni itaimba kwa furaha. 13 Mbele za Baba yetu, kwa maana anakuja, kwa maana anakuja kuihukumu dunia. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, na watu kwa uaminifu wake.