Yerusalemu Katika Magofu
Zaburi ya Asafu.
79 1 Baba yetu, mataifa yameuvamia urithi wako; wamelinajisi hekalu lako takatifu; wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.
2 Wametoa maiti za watumishi wako ziwe chakula cha ndege wa angani, nyama ya waaminifu wako kwa wanyama wa nchi. 3 Wamemwaga damu yao kama maji pande zote za Yerusalemu, wala hakuna wa kuwazika. 4 Tumekuwa kitu cha kudharauliwa kwa jirani zetu, tunadhihakiwa na kufanyiwa mzaha na wale wanaotuzunguka.
5 Hata lini, Baba yetu? Je, utakasirika milele? Je, wivu wako utawaka kama moto? 6 Mimina ghadhabu yako juu ya mataifa yasiyokujua wewe, na juu ya falme zisizoliitia jina lako. 7 Kwa maana wamemla Yakobo na kuiharibu nchi yake. 8 Usituhesabie dhambi za baba zetu; huruma yako ya upole na itujie upesi kutulaki, kwa maana tumeshushwa chini sana.
9 Utusaidie, Baba yetu utuokoaye, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; utuokoe na kuzifunika dhambi zetu kwa ajili ya jina lako. 10 Kwa nini mataifa waseme, "Yuko wapi Mungu wao?" Mbele ya macho yetu, na ijulikane katika mataifa ya kuwa unatenda haki kwa ajili ya damu ya watumishi wako iliyomwagwa. 11 Kilio cha mfungwa na kifike mbele zako; kwa ukuu wa mkono wako, uwahifadhi wale waliohukumiwa kufa.
12 Uwalipe jirani zetu mara saba vifuani mwao dhihaka waliyokudhihaki wewe, Ee Baba Mwenye Enzi. 13 Ndipo sisi, watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakushukuru milele; toka kizazi hata kizazi tutazitangaza sifa zako.