Kukuonea Kiu Wewe
Zaburi ya Daudi, alipokuwa katika jangwa la Yuda.
63 1 Baba yangu, wewe ndiwe Baba yangu; nakutafuta kwa moyo wangu wote. Nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu wote unakutamani, katika nchi kame na yenye uchovu isiyokuwa na maji. 2 Hivyo nimekutazama katika patakatifu na kuuona uweza wako na utukufu wako. 3 Kwa kuwa upendo wako wa agano ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakusifu. 4 Hivyo nitakubariki maadamu ninaishi; kwa jina lako nitainua mikono yangu. 5 Nafsi yangu inashiba kama kwa vyakula vinono, na kwa midomo yenye furaha kinywa changu kinakusifu.
6 Ninapokukumbuka kitandani mwangu, na kukutafakari katika masaa marefu ya usiku. 7 Kwa kuwa umekuwa msaada wangu, na katika uvuli wa mbawa zako naimba kwa furaha. 8 Nafsi yangu inashikamana nawe; mkono wako wa kuume unanishika imara.
9 Lakini wale watafutao kuangamiza uhai wangu watashuka pande za chini za nchi. 10 Watatolewa kwa upanga; watakuwa chakula cha mbweha. 11 Lakini mfalme atafurahi katika Baba yetu; wote waapao kwa Baba yetu watashangilia, kwa kuwa vinywa vya waongo vitanyamazishwa.