Nafsi Yenye Kiu
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya hekima ya wana wa Kora.
42 1 Kama ayala aoneavyo shauku vijito vya maji, ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku wewe, Baba yangu.
2 Nafsi yangu inamwonea kiu Baba yangu, Baba aliye hai. Ni lini nitakapokuja na kuonekana mbele zake? 3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, hali wakiniambia mchana kutwa, "Yuko wapi Mungu wako?"
4 Mambo haya nayakumbuka, ninapoimimina nafsi yangu: jinsi nilivyokuwa nikienda pamoja na umati na kuwaongoza katika msafara mpaka nyumba ya Baba yetu, kwa vigelegele vya furaha na nyimbo za sifa, umati mkubwa ukisherehekea.
5 Kwa nini unasononeka, nafsi yangu, na kwa nini unafadhaika ndani yangu? Umtumaini Baba yetu; kwa maana nitamsifu tena, wokovu wangu na Baba yangu.
6 Baba yangu, nafsi yangu imesononeka ndani yangu; kwa hiyo nakukumbuka wewe toka nchi ya Yordani na ya Hermoni, toka mlima Mizari.
7 Kilindi kinaita kilindi kwa mshindo wa maporomoko yako ya maji; maji yako yote na mawimbi yako yamepita juu yangu. 8 Mchana Baba yetu huamuru upendo wake wa agano, na usiku wimbo wake u pamoja nami, sala kwa Baba wa uzima wangu.
9 Namwambia Baba yangu, mwamba wangu, "Mbona umenisahau mimi? Mbona ninakwenda nikiomboleza kwa sababu ya kuonewa na adui?" 10 Kama jeraha la kuua mifupani mwangu, watesi wangu wananidhihaki mimi, hali wakiniambia mchana kutwa, "Yuko wapi Mungu wako?"
11 Kwa nini unasononeka, nafsi yangu, na kwa nini unafadhaika ndani yangu? Umtumaini Baba yetu; kwa maana nitamsifu tena, wokovu wangu na Baba yangu.