Uzito wa Dhambi Yangu
Zaburi ya Daudi, ya kukumbusha.
Akiwa mgonjwa, vidonda vyake vikitunga usaha, ameachwa na rafiki zake wakati adui wanapanga shauri, Daudi hufuatilia hali yake hadi dhambi yake mwenyewe, wala hajibizani na wamshtakio. Hunyamaza kama kiziwi na humngoja Baba yake, yeye peke yake anayemtazamia kumjibu.
38 1Ee Baba yangu, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. 2Kwa maana mishale yako imezama ndani yangu, na mkono wako umenishukia kwa nguvu. 3Hakuna uzima katika mwili wangu kwa sababu ya hasira yako; hakuna afya katika mifupa yangu kwa sababu ya dhambi yangu.
4Kwa maana dhambi zangu zimefurika juu ya kichwa changu; kama mzigo mzito, zimenilemea kupita kiasi. 5Vidonda vyangu vinanuka na kutunga usaha kwa sababu ya upumbavu wangu. 6Nimepindika na kuinama chini kabisa; mchana kutwa naenda nikiomboleza. 7Kwa maana viuno vyangu vimejaa mwako, na hakuna afya katika mwili wangu.
8Nimekufa ganzi na kupondwa kabisa; naugua kwa sababu ya machafuko ya moyo wangu. 9Ee Baba yangu Mwenye Enzi, shauku yangu yote iko mbele zako, na kuugua kwangu hakukufichika kwako. 10Moyo wangu unadunda, nguvu zangu zimeniishia; hata nuru ya macho yangu imeniondokea. 11Rafiki zangu na wenzangu wanajitenga na mateso yangu, na jamaa zangu wa karibu wanasimama mbali.
12Wanaoutafuta uhai wangu wanategemeza mitego yao; wanaotafuta madhara yangu wananena maangamizi na kupanga hila mchana kutwa. 13Lakini mimi ni kama kiziwi asiyeweza kusikia, kama asiyeweza kunena wala hafumbui kinywa chake. 14Nimekuwa kama mtu asiyesikia, asiye na jibu kinywani mwake. 15Lakini nakungoja wewe, Baba yangu; ni wewe utakayenijibu, Ee Baba yangu Mwenye Enzi.
16Kwa maana nilisema, "Wasije wakanishangilia kamwe—wale wanaojigamba juu yangu wakati mguu wangu utelezapo." 17Kwa maana niko tayari kuanguka, na maumivu yangu yako mbele yangu daima. 18Naungama uovu wangu; nataabika kwa sababu ya dhambi yangu. 19Lakini adui zangu wana nguvu na wamejaa uhai, na wengi ni wale wanaonichukia bila sababu.
20Wale wanaonilipa maovu badala ya mema wananishitaki kwa sababu nafuatia yaliyo mema. 21Usiniache, Baba yangu; usisimame mbali nami, Baba yangu. 22Fanya haraka kunisaidia, Ee Baba yangu Mwenye Enzi, wokovu wangu.