Mkate Juu ya Maji
Tupa mkate wako juu ya maji na ugawe fungu lako kwa wengi, kwa maana hujui msiba gani unakuja. Yeye aitazamaye upepo hapandi kamwe. Panda asubuhi na jioni, ifurahie nuru, uzikumbuke siku za giza zijazo, na ujue kwamba Mungu atauleta ujana hukumuni.
11 1Tupa mkate wako juu ya maji, kwa maana baada ya siku nyingi utaupata tena. 2Toa fungu kwa saba, au hata kwa nane, kwa maana hujui msiba gani utakaoijia nchi. 3Mawingu yakijaa, hunyesha mvua juu ya nchi; na mti ukianguka kusini au kaskazini, mahali pale uangukapo, hapo ndipo utakapolala. 4Yeye aitazamaye upepo hatapanda kamwe, na yeye ayaangaliaye mawingu hatavuna kamwe.
5Kama vile usivyojua njia ya upepo, wala jinsi mifupa inavyoumbika tumboni mwa mwanamke mwenye mimba, kadhalika huwezi kuijua kazi ya Mungu, yeye afanyaye vitu vyote.
6Panda mbegu yako asubuhi, na jioni usiuzuie mkono wako, kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa—hii au ile—au kama zote mbili zitafanya vyema sawasawa.
Nuru ni Tamu
7Nuru ni tamu, nako ni kupendeza kwa macho kuliona jua.
8Basi mtu akiishi miaka mingi, na afurahi katika hiyo yote; lakini na azikumbuke siku za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Kila kijacho ni ubatili.
9Furahi, ewe kijana, katika ujana wako, na moyo wako ukupe furaha katika siku za ujana wako. Enenda katika njia za moyo wako na katika kuona kwa macho yako; lakini ujue ya kuwa kwa ajili ya mambo haya yote Mungu atakuleta hukumuni.
10Basi ondoa masikitiko moyoni mwako, na uutenge mbali maumivu na mwili wako, kwa maana ujana na mapambazuko ya maisha ni ubatili.