Bado Mnakua Katika Baba
Wakorintho wanagawanyika katika vikundi vya mashabiki—mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo—naye Paulo analiita hilo utoto. Apandaye na atiaye maji si kitu; Baba yetu ndiye akuzaye. Kila mtu ajengalo juu ya ule msingi mmoja litadhihirishwa kwa moto.
3 1Ndugu zangu, sikuweza kusema nanyi kama watu wa Roho, bali kama watu wa mwili—watoto wachanga katika Kristo. 2Naliwanywesha maziwa, si chakula kigumu, kwa maana mlikuwa hamjaweza kukipokea. Naam, hata sasa hamjaweza, 3kwa maana bado ninyi ni watu wa mwili. Kwa kuwa palipo na wivu na ugomvi kati yenu, je! ninyi si watu wa mwili, mnaoenenda kwa kawaida ya wanadamu? 4Kwa maana mmoja asemapo, "Mimi ni wa Paulo," na mwingine, "Mimi ni wa Apolo," je! ninyi si wanadamu tu?
5Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni watumishi ambao kwao mliamini, kila mmoja kama Bwana alivyompa. 6Mimi nalipanda, Apolo alitia maji, bali Baba yetu ndiye aliyekuza. 7Basi, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Baba yetu akuzaye. 8Apandaye na atiaye maji ni wamoja; na kila mmoja atapata thawabu yake mwenyewe kwa kadiri ya taabu yake mwenyewe. 9Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Baba yetu; ninyi ni shamba lake, ni jengo lake.
10Kwa kadiri ya neema ya Baba yetu niliyopewa, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima naliweka msingi, na mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. 11Kwa maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. 12Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo dhahabu, au fedha, au mawe ya thamani, au miti, au majani, au manyasi, 13kila mtu kazi yake itakuwa dhahiri; maana ile Siku itaidhihirisha, kwa sababu moto ndio uifunuao, na moto uleule utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. 14Kazi ya mtu aliyoijenga ikidumu, atapata thawabu. 15Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini ni kama kwa kupitia motoni.
16Hamjui ya kuwa ninyi ni hekalu la Baba yetu, na ya kuwa Roho wa Baba yetu anakaa ndani yenu? 17Mtu akiliharibu hekalu la Baba yetu, Baba yetu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Baba yetu ni takatifu, ambalo ni ninyi.
18Mtu asijidanganye mwenyewe. Kama mtu ye yote miongoni mwenu akijiona kuwa ni mwenye hekima katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa na hekima. 19Kwa maana hekima ya dunia hii ni upumbavu mbele za Baba yetu. Kwa maana imeandikwa, "Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao," 20na tena, "Baba yetu anayajua mawazo ya wenye hekima, ya kuwa ni ubatili." 21Basi mtu asijisifu kwa wanadamu. Kwa maana vitu vyote ni vyenu; 22ikiwa Paulo, au Apolo, au Kefa, au dunia, au uzima, au mauti, au vilivyopo, au vitakavyokuwapo—vyote ni vyenu, 23nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Baba yetu.