Heshima katika Ibada na Utaratibu
Matatizo mawili katika kusanyiko: vichwa vilivyofunikwa au visivyofunikwa wakati wa kumwomba Baba yetu, na Meza ya Bwana ambapo matajiri wanakula kwanza hali maskini wanakaa na njaa. Hilo la mwisho ndiyo sababu baadhi ni dhaifu na wagonjwa—wanakula pasipo kuutambua mwili. Ngojeaneni.
11 1Iweni wafuasi wangu, kama mimi nami nilivyo wa Kristo.
2Basi nawasifu kwa kunikumbuka katika kila jambo na kuyashika mapokeo kama nilivyowakabidhi. 3Nataka mjue: kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Baba yetu. 4Kila mwanamume anayeomba au kutoa unabii hali kichwa chake kimefunikwa, hukivunjia heshima kichwa chake. 5Lakini kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii hali kichwa chake hakijafunikwa, hukivunjia heshima kichwa chake—ni sawa na kunyolewa nywele. 6Kama mwanamke akikataa kufunika kichwa chake, na akatwe nywele; lakini kwa kuwa ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele au kunyolewa, na afunike kichwa chake. 7Mwanamume haimpasi kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano na utukufu wa Baba yetu; naye mwanamke ni utukufu wa mwanamume. 8Kwa maana mwanamume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanamume. 9Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume. 10Kwa hiyo mwanamke imempasa kuwa na ishara ya mamlaka juu ya kichwa chake, kwa sababu ya malaika.
11Walakini, katika Bwana mwanamke hajitegemei bila mwanamume, wala mwanamume hajitegemei bila mwanamke. 12Kwa maana kama mwanamke alivyotoka kwa mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa kwa mwanamke; na vitu vyote vyatoka kwa Baba yetu. 13Amueni ninyi wenyewe: je, ni vyema mwanamke amwombe Baba yetu hali kichwa chake hakijafunikwa? 14Je, hata asili yenyewe haiwafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni fedheha kwake, 15bali mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Kwa maana amepewa hizo nywele ziwe kifuniko chake. 16Lakini mtu ye yote akitaka kushindana kwa neno hili, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Baba yetu.
Meza ya Bwana Yavunjiwa Heshima
17Nami katika kutoa agizo hili, siwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa faida bali kwa hasara. 18Kwanza, mkutanikapo kama kanisa, nasikia kwamba kuna mafarakano kati yenu; nami nusu naamini. 19Kwa maana lazima kuwe na mafarakano kati yenu, ili wale waliohalisi kati yenu wapate kudhihirika. 20Basi, mnapokutanika mahali pamoja, si Meza ya Bwana mnayoila. 21Kwa maana mnapokula, kila mmoja hutangulia kula chakula chake mwenyewe—mmoja ana njaa, na mwingine amelewa. 22Je, hamna nyumba za kulia na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Baba yetu, na kuwaaibisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? Katika jambo hili siwasifu.
23Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana yale niliyowakabidhi ninyi: ya kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliotolewa, alitwaa mkate,
24naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, "Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu." 25Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, "Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu."
26Kwa maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mnaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
27Basi kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya mwili na damu ya Bwana. 28Lakini mtu ajichunguze mwenyewe, ndipo aule mkate na kukinywa kikombe. 29Kwa maana ye yote alaye na kunywa pasipo kuupambanua mwili, hujilia na hujinywea hukumu. 30Kwa sababu hiyo wako wengi kati yenu walio hawawezi na wagonjwa, na kadhaa wamelala usingizi. 31Lakini kama tungejihukumu wenyewe kwa haki, tusingehukumiwa. 32Bwana anapotuhukumu, hutuadhibu, ili tusipate kuhukumiwa pamoja na dunia. 33Basi, ndugu zangu, mkutanikapo ili kula, ngojaneni. 34Mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutanika kwenu kusilete hukumu. Na mambo yaliyosalia nitayatengeneza nitakapokuja.