Mpango wa Naomi
3 1Kisha Naomi, mama-mkwe wake, akamwambia, "Binti yangu, je, nisikutafutie makao ili upate raha? 2Je, Boazi, ambaye ulikuwa pamoja na wanawake wake vijana, si jamaa yetu? Usiku wa leo anapepeta shayiri kwenye sakafu ya kupuria. 3Oga, ujipake marashi, uvae vazi lako, kisha ushuke kwenda kwenye sakafu ya kupuria. Usijionyeshe kwa mtu huyo hata atakapomaliza kula na kunywa. 4Atakapolala, uangalie mahali alalapo; kisha uende ufunue miguu yake na ulale hapo—naye atakuambia utakalofanya."
5Naye Ruthu akamwambia, "Yote unayosema nitayafanya." 6Basi akashuka kwenda kwenye sakafu ya kupuria, akafanya kila kitu ambacho mama-mkwe wake alimwambia. 7Boazi akala, akanywa, akajisikia vizuri moyoni mwake, kisha akalala pembeni mwa chungu cha nafaka. Naye akaja kwa siri, akafunua miguu yake, akalala hapo. 8Usiku wa manane mtu yule akashtuka, akageuka, na tazama, mwanamke amelala miguuni pake! 9"Wewe ni nani?" akauliza. "Mimi ni Ruthu, mtumishi wako," akajibu. "Tandaza pindo la vazi lako juu ya mtumishi wako, kwa maana wewe ni mkombozi." a a v9 Kutandaza pindo la vazi juu ya mtu ilikuwa ni ombi la ndoa na ulinzi.
10Akasema, "Umebarikiwa na Baba yetu, binti yangu. Fadhili hii ya mwisho ni bora kuliko ile ya kwanza, kwa kuwa hukuwafuata vijana wanaume, maskini au tajiri. 11Sasa, binti yangu, usiogope. Nitakufanyia yote unayoyaomba, kwa maana mji wangu wote wajua ya kuwa wewe ni mwanamke mwenye sifa njema. 12Sasa ni kweli kwamba mimi ni mkombozi, lakini yuko mkombozi aliye wa karibu zaidi kuliko mimi. 13Kaa usiku wa leo. Asubuhi, kama atakukomboa—vyema, na akukomboe. Lakini kama hataki, basi kama aishivyo Baba yetu, mimi nitakukomboa. Lala hata asubuhi."
14Akalala miguuni pake hata asubuhi, akaondoka kabla mtu hajaweza kumtambua mwenzake, kwa maana alisema, "Isijulikane ya kuwa mwanamke alikuja kwenye sakafu ya kupuria." 15Akasema, "Lete shela uliyoivaa; uinyoshe." Naye akainyosha. Akapima vipimo sita vya shayiri, akamtwika, kisha akaingia mjini.
16Ruthu alipofika kwa mama-mkwe wake, Naomi akauliza, "Ilikuwaje, binti yangu?" Naye akamweleza yote ambayo mtu yule alimtendea. 17Akasema, "Alinipa vipimo hivi sita vya shayiri, akisema, 'Usirudi kwa mama-mkwe wako mikono mitupu.'"
18Naomi akasema, "Ngoja, binti yangu, hata utakapojua litakalotokea, kwa maana mtu yule hatatulia hata atakapolimaliza jambo hili leo."