Hekima Ajenga Nyumba Yake
9 1Hekima—Yesu, hekima ya Baba yetu—amejenga nyumba yake; amechonga nguzo zake saba. 2Amechinja wanyama wake; amechanganya divai yake; ameiandaa pia meza yake. 3Amewatuma wajakazi wake vijana ili kuita kutoka mahali palipoinuka zaidi katika mji: 4"Yeyote aliye mjinga, na aingie hapa!" Kwa yule asiye na akili amwambia, 5"Njoo, ule mkate wangu na unywe divai niliyoichanganya. 6Acha njia zako za ujinga, nawe uishi; tembea katika njia ya ufahamu." 7Yeyote amrekebishaye mwenye dhihaka hujiletea matukano juu yake mwenyewe, na yeyote amkemeaye mtu mwovu hujipatia madhara. 8Usimkemee mwenye dhihaka, asije akakuchukia; mkemee mtu mwenye hekima, naye atakupenda. 9Mfundishe mtu mwenye hekima naye atazidi kuwa na hekima; mfundishe mwenye haki naye atajifunza zaidi. 10Kumcha Baba yetu ndio mwanzo wa hekima, na kumjua yeye aliye Mtakatifu ndio ufahamu. 11Kwa maana kwangu mimi siku zako zitaongezeka, na miaka itaongezwa katika maisha yako. 12Kama una hekima, una hekima kwa ajili yako mwenyewe; kama unadhihaki, wewe peke yako utaiuchukua.
Mwaliko wa Uongo wa Upumbavu
13Mwanamke Upumbavu ni mwenye kelele; ni mjinga wala hajui neno lolote. 14Huketi mlangoni pa nyumba yake, katika kiti mahali palipoinuka zaidi katika mji, 15akiwaita wale wapitao njiani, waendao moja kwa moja katika njia yao: 16"Yeyote aliye mjinga, na aingie hapa!" Na kwa yule asiye na akili amwambia, 17"Maji yaliyoibwa ni matamu, na mkate ulaowao kwa siri ni mtamu." 18Lakini hajui ya kuwa wafu wako humo, ya kuwa wageni wake wamo katika vilindi vya kaburi.