Itafute Kama Fedha
2 1Mwanangu, kama ukiyapokea maneno yangu na kuzihifadhi amri zangu ndani yako, 2ukitega sikio lako kusikia hekima na kuuelekeza moyo wako upate ufahamu; 3naam, kama ukiuombea busara na kupaza sauti yako upate ufahamu, 4kama ukiitafuta kama fedha na kuiwinda kama hazina iliyofichwa, 5ndipo utakapofahamu kumcha Baba yetu na kupata maarifa ya kumjua Baba yetu. 6Kwa maana Baba yetu hutoa hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. 7Huwawekea wanyofu hekima ya kweli; ni ngao kwa wale waendao kwa ukamilifu, 8akizilinda njia za haki na kuutunza mwenendo wa waaminifu wake.
9Ndipo utakapofahamu haki na hukumu ya adili na unyofu—kila njia njema. 10Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yatakuwa matamu nafsini mwako; 11busara itakulinda, na ufahamu utakuhifadhi, 12ukikuokoa na njia ya uovu, na watu wanenao yaliyopotoka, 13waziachao njia za unyofu ili waende katika njia za giza, 14wafurahiao kutenda mabaya na kushangilia upotovu wa uovu, 15ambao njia zao zimepotoka, na ambao ni wakaidi katika mienendo yao.
16Hekima itakuokoa pia na yule mwanamke mgeni, na yule mgeni mwenye maneno laini, 17amwachaye mwenzi wa ujana wake na kulisahau agano la Baba yake. 18Kwa maana nyumba yake huzama kufikia mautini, na njia zake huelekea kwa waliokufa. 19Hakuna aendaye kwake arudiye, wala hawazifikii njia za uzima.
20Basi utakwenda katika njia ya watu wema na kuzishika njia za wenye haki. 21Kwa maana wanyofu watakaa katika nchi, na wakamilifu watabaki ndani yake; 22bali waovu watakatiliwa mbali na nchi, na wadanganyifu watang'olewa ndani yake.