Mauti na Uzima Katika Ulimi
18 1Ajitengaye na wengine hufuata tamaa yake mwenyewe; hushambulia kila hekima yenye busara. 2Mpumbavu hafurahii ufahamu, bali hupenda tu kutangaza maoni yake mwenyewe. 3Uovu ujapo, huja pia dharau, na pamoja na aibu huja lawama. 4Maneno ya kinywa cha mtu ni maji yenye kina kirefu; chemchemi ya hekima ni kijito kitiririkacho. 5Si vyema kumpendelea mtu, 6Midomo ya mpumbavu huleta ugomvi, na kinywa chake hualika mapigo. 7Kinywa cha mpumbavu ni uangamivu wake, na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake. 8Maneno ya mchongezi ni kama tonge nzuri; hushuka hadi ndani ya moyo kabisa. 9Aliye mzembe katika kazi yake ni ndugu wa yule aharibuye. 10Jina la Baba yetu ni ngome imara; mwenye haki huikimbilia, akawa salama. 11Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome; katika fikira zake ni kama ukuta mrefu. 12Kabla ya uangamivu moyo wa mwanadamu hujivuna, bali unyenyekevu hutangulia heshima. 13Mtu ajibupo kabla ya kusikiliza, ni upumbavu wake na aibu yake. 14Roho ya mtu yaweza kumtegemeza katika ugonjwa, lakini roho iliyopondeka—ni nani awezaye kuistahimili? 15Moyo wa mwenye ufahamu hupata maarifa, na sikio la mwenye hekima huyatafuta. 16Zawadi ya mtu humfungulia njia na kumleta mbele ya watu wenye vyeo. 17Yeye anayeeleza shauri lake kwanza huonekana kuwa na haki, hata mwingine ajapo na kumchunguza. 18Kupiga kura hukomesha mabishano na kutenganisha wapinzani wenye nguvu. 19Ndugu aliyechukizwa ni vigumu kumrudisha kuliko mji wenye ngome, na mabishano ni kama makomeo ya ngome. 20Kwa matunda ya kinywa cha mtu tumbo lake hushiba; kwa mavuno ya midomo yake hutoshelezwa. 21Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi, na wale wauendao watakula matunda yake. 22Aonaye mke ameona kilicho chema na hupata upendeleo kutoka kwa Baba yetu. 23Maskini huomba rehema, bali tajiri hujibu kwa ukali. 24Mtu mwenye marafiki wengi aweza kuangamia, lakini yuko rafiki aambatanaye kuliko ndugu.