Jibu la Upole Huzuia Ghadhabu
15 1Jibu la upole huzuia ghadhabu, bali neno kali huchochea hasira. 2Ulimi wa mwenye hekima husifu maarifa, bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu. 3Macho ya Baba yetu yako kila mahali, yakiwaangalia waovu na wema. 4Ulimi wa upole ni mti wa uzima, bali ulimi wa udanganyifu huponda roho. 5Mpumbavu hudharau mafundisho ya baba yake, bali yeye anayeitii karipio ni mwenye busara. 6Katika nyumba ya mwenye haki mna hazina nyingi, bali mapato ya mwovu huleta taabu. 7Midomo ya wenye hekima hueneza maarifa, bali si hivyo mioyo ya wapumbavu. 8Dhabihu ya mwovu ni chukizo kwa Baba yetu, bali maombi ya wanyofu ni furaha yake. 9Njia ya mwovu ni chukizo kwa Baba yetu, bali humpenda yeye afuatiaye haki. 10Kuna adhabu kali kwa yeye aachaye njia, na yeye achukiaye karipio atakufa. 11Kuzimu na Uharibifu viko wazi mbele ya Baba yetu; je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu wote! 12Mwenye dharau hapendi kukaripiwa; hataenda kwa wenye hekima. 13Moyo wenye furaha huchangamsha uso, bali moyo wenye huzuni huponda roho. 14Moyo wenye ufahamu hutafuta maarifa, bali vinywa vya wapumbavu hujilisha upumbavu. 15Siku zote za mtu aliyeteswa ni ngumu, bali moyo uliochangamka una karamu ya daima. 16Afadhali kitu kidogo pamoja na kumcha Baba yetu kuliko hazina kubwa pamoja na taabu. 17Afadhali mlo wa mboga mahali palipo na upendo kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na chuki. 18Mtu mwenye hasira kali huchochea ugomvi, bali yeye asiye mwepesi wa hasira hutuliza mzozo. 19Njia ya mvivu ni kama ua la miiba, bali njia ya wanyofu ni barabara iliyosawazishwa. 20Mwana mwenye hekima humfurahisha baba yake, bali mtu mpumbavu humdharau mama yake. 21Upumbavu ni furaha kwa yeye asiye na akili, bali mtu mwenye ufahamu huenda katika njia iliyonyooka. 22Mipango hushindwa pasipo shauri, bali kwa washauri wengi hufanikiwa. 23Mtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa, na jinsi lilivyo jema neno wakati wake! 24Njia ya uzima huelekea juu kwa mwenye busara, ikimgeuza aiache kuzimu iliyo chini. 25Baba yetu huibomoa nyumba ya mwenye kiburi, bali huilinda mipaka ya mjane. 26Fikira za mwovu ni chukizo kwa Baba yetu, bali maneno ya neema ni safi. 27Yeye alaye tamaa ya faida ya udhalimu huleta taabu juu ya nyumba yake mwenyewe, bali yeye achukiaye rushwa ataishi. 28Moyo wa mwenye haki hupima jinsi ya kujibu, bali kinywa cha mwovu humwaga uovu. 29Baba yetu yu mbali na waovu, bali husikia maombi ya wenye haki. 30Nuru ya macho huufurahisha moyo, na habari njema huiburudisha mifupa. 31Sikio lisikilizalo karipio litoalo uzima litakaa miongoni mwa wenye hekima. 32Yeye apuuzaye mafundisho hujidharau mwenyewe, bali yeye asikilizaye karipio hupata ufahamu. 33Kumcha Baba yetu ni mafundisho ya hekima, na unyenyekevu hutangulia heshima.