Kinara cha Taa
8 1Baba yetu akasema na Musa, akinena:
2"Nena na Haruni: Utakapoziwasha taa, zile saba zitatoa nuru mbele ya kinara."
3Haruni akafanya hivyo, akaziwasha taa zake ili zitoe nuru kuelekea upande wa mbele wa kinara, kama Baba yetu alivyomwamuru Musa. 4Kazi ya kinara ilikuwa: dhahabu iliyofuliwa, iliyofuliwa toka tako hata maua yake—kilifanywa sawasawa kabisa kama Baba yetu alivyomwonyesha Musa.
Waliotengwa kwa ajili ya Baba yetu
5Baba yetu akasema na Musa, akinena:
6"Watwae Walawi toka miongoni mwa wana wa Israeli, na kuwatakasa. 7Ili kuwatakasa, fanya hivi: nyunyiza maji ya utakaso juu yao, pitisha wembe juu ya mwili wao wote, waoshe nguo zao, nao watakuwa safi. a a v7 Maji ya utakaso yalikuwa maji maalumu ya kutakasa yaliyotumika katika kuwatenga Walawi, yakiwaonyesha kuwa wamefanywa safi ili kutumika mbele za Baba yetu. 8Nao watwae ng'ombe mume mchanga kutoka kundini, pamoja na sadaka yake ya unga laini uliochanganywa na mafuta; nawe utatwaa ng'ombe mume mchanga wa pili kutoka kundini kwa ajili ya sadaka ya dhambi. 9Uwalete Walawi mbele ya hema ya kukutania, na kuukusanya mkutano wote wa wana wa Israeli. 10Utakapowaleta Walawi mbele zangu, wana wa Israeli wataweka mikono yao juu ya Walawi, 11na Haruni atawatikisa Walawi mbele zangu kuwa sadaka ya kutikiswa itokayo kwa wana wa Israeli, ili wapate kuitumikia kazi ya Baba yetu. 12Kisha Walawi wataweka mikono yao juu ya vichwa vya wale ng'ombe; utamtoa mmoja kuwa sadaka ya dhambi na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa kwangu, ili kuwafanyia Walawi upatanisho. 13Utawasimamisha Walawi mbele ya Haruni na wanawe, na kuwatoa kwangu kuwa sadaka ya kutikiswa. 14Utawatenga Walawi toka miongoni mwa wana wa Israeli, nao Walawi watakuwa wangu. 15Kisha baada ya hayo Walawi wataingia kuitumikia hema ya kukutania, hapo utakapokwisha kuwatakasa na kuwatoa kuwa sadaka ya kutikiswa. 16Kwa maana wametolewa kwangu kabisa toka miongoni mwa wana wa Israeli; badala ya kila afunguaye tumbo, mzaliwa wa kwanza wa wote wa wana wa Israeli, nimewatwaa wawe wangu. 17Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote wa wana wa Israeli ni wangu, wa binadamu na wa wanyama; siku ile nilipowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, niliwatenga wawe wangu. 18Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote miongoni mwa wana wa Israeli. 19Nami nimewatoa Walawi kuwa zawadi kwa Haruni na wanawe toka miongoni mwa wana wa Israeli, ili wawatumikie wana wa Israeli katika hema ya kukutania, na kuwafanyia wana wa Israeli upatanisho, ili pasiwe na pigo juu ya wana wa Israeli watakapoukaribia mahali patakatifu."
20Basi Musa, na Haruni, na mkutano wote wa wana wa Israeli, wakawafanyia Walawi kama yote Baba yetu alivyomwamuru Musa katika habari za Walawi; ndivyo wana wa Israeli walivyowafanyia. 21Nao Walawi wakajitakasa na dhambi, wakazifua nguo zao; Haruni akawatoa kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za Baba yetu, akawafanyia upatanisho ili kuwatakasa. 22Baada ya hayo, Walawi wakaingia kuitumikia kazi yao katika hema ya kukutania mbele ya Haruni na wanawe; kama Baba yetu alivyomwamuru Musa katika habari za Walawi, ndivyo walivyowafanyia.
23Baba yetu akasema na Musa, akinena:
24"Hili ndilo lihusulo Walawi: tangu umri wa miaka ishirini na mitano, watakuja kuitumikia kazi katika hema ya kukutania. 25Na tangu umri wa miaka hamsini watastaafu katika kazi ya utumishi, wala hawatatumika tena. 26Wataweza kuwasaidia ndugu zao katika hema ya kukutania kwa kulinda zamu, lakini hawatafanya kazi. Hivyo ndivyo utakavyowagawia Walawi kazi zao."