Adui Wanaidhihaki Kazi
4 1Sanballati aliposikia kwamba tunaujenga upya ukuta, alighadhibika na kujawa na hasira kali, akawadhihaki Wayahudi. 2Akasema mbele ya ndugu zake na jeshi la Samaria, "Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, wataurejesha ukuta kwa ajili yao wenyewe? Je, watatoa dhabihu? Je, watamaliza kwa siku moja? Je, wanaweza kuyafufua mawe kutoka kwenye marundo ya kifusi, hali yakiwa yamechomeka?"
3Tobia Mwamoni alikuwa kando yake, akasema, "Ukuta huo wa mawe wanaoujenga—hata mbweha akipanda juu yake, ataubomoa!"
4Utusikie, Baba yetu, kwa maana tumedharauliwa. Zirudishe dhihaka zao juu ya vichwa vyao wenyewe, na uwatoe wawe nyara katika nchi ya utumwa. 5Usiuache uovu wao, wala usiiache dhambi yao ifutwe mbele za macho yako, kwa maana wamewatukana wajenzi machoni pao.
6Basi tuliujenga upya ukuta hata wote ukaunganishwa mpaka nusu ya kimo chake, kwa maana watu walifanya kazi kwa moyo wao wote.
7Lakini Sanballati, Tobia, Waarabu, Waamoni, na Waashdodi waliposikia kwamba ukarabati wa kuta za Yerusalemu ulikuwa unaendelea na mianya ilikuwa inaanza kuzibwa, walijawa na hasira. 8Wote wakapanga shauri pamoja kuja kupigana na Yerusalemu na kuivuruga.
9Lakini tulimwomba Baba yetu, tukaweka walinzi dhidi yao mchana na usiku.
10Wakati huo huo watu wa Yuda wakasema, "Wafanyakazi wanaishiwa nguvu zao, na kuna kifusi kingi mno hata hatuwezi kuujenga upya ukuta." 11Na adui zetu wakasema, "Kabla hawajajua wala kutuona, tutakuwa katikati yao; tutawaua na kuikomesha kazi."
12Ndipo Wayahudi walioishi karibu nao wakaja na kutuambia mara kumi, "Popote mgeukiapo, watakuja juu yetu."
13Basi niliwaweka watu nyuma ya sehemu za chini kabisa za ukuta, katika mahali palipo wazi, nikiwapanga kwa jamaa zao pamoja na panga zao, mikuki yao, na pinde zao. 14Baada ya kuyaangalia mambo, nilisimama nikawaambia wakuu, na maafisa, na watu wengine waliobaki, "Msiwaogope. Mkumbukeni Baba Mwenye Enzi, aliye mkuu na wa kutisha, mkapigane kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu na binti zenu, wake zenu na nyumba zenu."
15Adui zetu waliposikia kwamba tumelijua shauri lao na kwamba Baba yetu amelibatilisha, sote tukarudi ukutani, kila mtu kwenye kazi yake. 16Tangu siku ile na kuendelea, nusu ya watu wangu walifanya kazi, na nusu nyingine walikuwa na mikuki, ngao, pinde, na mavazi ya vita. Maofisa walijiweka nyuma ya watu wote wa Yuda, 17waliokuwa wakiujenga ukuta. Wale waliobeba vifaa walifanya kazi yao kwa mkono mmoja, na kwa mkono mwingine walishika silaha, 18na kila mmoja wa wajenzi alikuwa amejifunga upanga wake kiunoni alipofanya kazi. Lakini mtu aliyepiga tarumbeta alikaa kando yangu. 19Kisha nikawaambia wakuu, na maafisa, na watu wengine waliobaki, "Kazi ni kubwa na imetapakaa, nasi tumetengana mmoja na mwenzake kando ya ukuta. 20Popote msikiapo sauti ya tarumbeta, kusanyikeni kwetu hapo. Baba yetu atapigana kwa ajili yetu!"
21Basi tuliendelea kufanya kazi, nusu ya watu wakishika mikuki, tangu mapambazuko ya alfajiri hata nyota zilipotokea. 22Wakati huo pia niliwaambia watu, "Kila mtu na msaidizi wake wakae ndani ya Yerusalemu usiku, ili wawe walinzi wakati wa usiku na wafanyakazi wakati wa mchana." 23Basi mimi, wala ndugu zangu, wala watu wangu, wala walinzi walionifuata, hatukuvua nguo zetu kamwe; kila mmoja alishika silaha yake mkononi, hata alipokwenda kuchota maji.