Soma. Pokea. Pendekeza.

♥ Maoni

Mambo ya Walawi 15

Kitabu

Baba yetu Anazungumza na Musa na Haruni

Sura ya 15.

Baba yetu akanena na Musa na Haruni, akisema:

"Semeni na wana wa Israeli, mkawaambie: Mtu ye yote akiwa na usaha unaotoka mwilini mwake, usaha wake ni najisi. Na huu ndio unajisi wake utokao kwa usaha wake: kama mwili wake unavuja usaha huo au umezuiwa, ni unajisi wake.

"Kila kitanda alaliacho mtu mwenye usaha huo ni najisi; na kila kitu akaliacho ni najisi. Na mtu ye yote akigusa kitanda chake, atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni. Na mtu ye yote aketiye juu ya kitu cho chote alichokalia yule mwenye usaha, atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni.

"Na mtu ye yote agusaye mwili wa yule mwenye usaha, atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni. Na yule mwenye usaha akimtemea mate mtu aliye safi, mtu huyo atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni.

"Na tandiko lo lote la kupanda alipandalo yule mwenye usaha litakuwa najisi. Na mtu ye yote agusaye kitu cho chote kilichokuwa chini yake atakuwa najisi hata jioni; na yeye achukuaye vitu hivyo atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni.

"Na mtu ye yote yule mwenye usaha amgusaye, iwapo hakunawa mikono yake kwa maji, atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni. Na chombo cho chote cha udongo akigusacho yule mwenye usaha kitavunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa kwa maji.

"Na hapo mwenye usaha atakapotakaswa na usaha wake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, atafua nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji yaliyo hai, naye atakuwa safi. Na siku ya nane atatwaa hua wawili au makinda mawili ya njiwa, atakuja mbele za Baba yetu penye mlango wa hema ya kukutania, na kuwatoa kwa kuhani. Na kuhani atawatoa, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Baba yetu kwa sababu ya usaha wake.

"Na mtu mume manii yakimtoka, ataosha mwili wake wote kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni. Na kila nguo, na kila ngozi, iliyo na manii juu yake, itaoshwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni. Na mwanamke ambaye mtu mume amelala naye kwa kutokwa na manii, watoga kwa maji wote wawili, nao watakuwa najisi hata jioni.

"Na mwanamke akiwa na kutoka damu mwilini mwake, kutoka huko kwa damu ni katika mwili wake, atakuwa katika unajisi wake wa hedhi siku saba; na mtu ye yote amgusaye atakuwa najisi hata jioni. Na kila kitu alaliacho katika unajisi wake kitakuwa najisi; na kila kitu akaliacho kitakuwa najisi. Na mtu ye yote agusaye kitanda chake atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni. Na mtu ye yote agusaye kitu cho chote akaliacho atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni. Tena kama ni juu ya kitanda, au juu ya kitu cho chote akaliacho, hapo akigusa mtu atakuwa najisi hata jioni.

"Na mtu mume akilala naye, na unajisi wake wa hedhi ukiwa juu yake, atakuwa najisi siku saba; na kila kitanda alaliacho kitakuwa najisi.

"Na mwanamke akitokwa na damu siku nyingi zisizokuwa za wakati wa hedhi yake, au akitokwa na damu zaidi ya wakati wa hedhi yake, siku zote za kutokwa kwake unajisi atakuwa kama katika siku za hedhi yake; yeye ni najisi. Kila kitanda alaliacho katika siku zote za kutoka kwake damu kitakuwa kwake kama kitanda cha hedhi yake; na kila kitu akaliacho kitakuwa najisi, kama unajisi wa hedhi yake. Na mtu ye yote avigusaye vitu hivyo atakuwa najisi; naye atafua nguo zake, na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi hata jioni.

"Lakini akitakaswa na kutoka kwake damu, atajihesabia siku saba, na baada ya hayo atakuwa safi. Na siku ya nane atatwaa hua wawili au makinda mawili ya njiwa, na kuwaleta kwa kuhani, penye mlango wa hema ya kukutania. Na kuhani atamtoa mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Baba yetu kwa sababu ya kutoka kwake unajisi.

"Ndivyo mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao, wasije wakafa katika unajisi wao, hapo watakapoinajisi maskani yangu iliyo kati yao.

"Hii ndiyo sheria yake yeye mwenye usaha, na yake yeye ambaye manii yamemtoka na kumtia unajisi; na yake yeye aliye mgonjwa kwa hedhi yake, na yake yeye mwenye usaha, mume au mke, na yake yeye alalaye na mwanamke aliye najisi."

A young man reading the Father's Heart Bible print edition in a coffee shop Sasa Imechapishwa

Maoni

Mawazo, maswali, au neno ambalo sura hii imeliamsha ndani yako — lishiriki hapa. Kila maoni huweka jina lako kwenye Wall of Contributors.

Kusoma, kunakili na kushiriki ni wazi kwa kila mtu — huhitaji akaunti. Kutoa maoni, kutia alama, na kuhifadhi mahali ulipofikia hupatikana kwa akaunti ya bure, na kila maoni huweka jina lako kwenye Wall of Contributors.

Jiunge na Familia — ni bure →
  • Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kuchangia.