Baba Anawainua Debora na Baraka
4 1Ehudi alipokwisha kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni pa Baba yetu. 2Kwa hiyo Baba yetu akawauza katika mkono wa Yabini mfalme wa Kanaani, aliyetawala katika Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi Haroshethi-ha-goimu. 3Ndipo Waisraeli wakamlilia Baba yetu, kwa maana Sisera alikuwa na magari ya chuma 900, naye alikuwa amewaonea kwa ukali kwa miaka ishirini. 4Basi Debora, mwanamke nabii, mke wa Lapidothi, alikuwa akiwaamua Israeli wakati ule. 5Alikuwa akikaa chini ya Mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya milima ya Efraimu; nao Waisraeli wakapanda kwake ili awahukumu. 6Akatuma watu wamwite Baraka mwana wa Abinoamu kutoka Kedeshi ya Naftali, akamwambia, "Je, Baba yetu, Mungu wa Israeli, hakukuamuru: Nenda, songa mpaka Mlima Tabori, ukachukue pamoja nawe watu 10,000 kutoka Naftali na Zabuloni. 7Nami nitamvuta Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, akutane nawe penye Mto Kishoni, pamoja na magari yake na majeshi yake, nami nitamtia mkononi mwako."
8Baraka akamwambia, "Kama ukienda pamoja nami, nitakwenda; lakini kama hutakwenda pamoja nami, sitakwenda."
9Akasema, "Hakika nitakwenda pamoja nawe; lakini hutapata utukufu katika njia utakayoiendea, kwa maana Baba yetu atamtia Sisera katika mkono wa mwanamke." Basi Debora akaondoka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi. 10Baraka akawaita Zabuloni na Naftali waje Kedeshi; watu 10,000 wakapanda nyuma yake, naye Debora akaenda pamoja naye. 11Basi Heberi Mkeni, mmoja wa wazao wa Hobabu, mkwe wa Musa, alikuwa amejitenga na Wakeni, akapiga hema yake mpaka mwaloni ulioko Saananimu, karibu na Kedeshi. 12Walipomwambia Sisera ya kwamba Baraka mwana wa Abinoamu amepanda Mlima Tabori, 13Sisera akayakusanya magari yake yote—magari ya chuma 900—na watu wake wote, kutoka Haroshethi-ha-goimu mpaka Mto Kishoni.
14Debora akamwambia Baraka, "Inuka! Leo Baba yetu anamtia Sisera mkononi mwako. Je, Baba yetu hakutangulia mbele yako?" Basi Baraka akashuka kwa kasi kutoka Mlima Tabori, akiwa na watu 10,000 nyuma yake. 15Naye Baba yetu akamfadhaisha Sisera, na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa upanga mbele ya Baraka; Sisera akaliacha gari lake, akakimbia kwa miguu. 16Baraka akayafuatia magari na jeshi mpaka Haroshethi-ha-goimu, na jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga; hakusalia mtu hata mmoja.
17Wakati huo Sisera akakimbia kwa miguu mpaka hema ya Yaeli, mke wa Heberi Mkeni, kwa maana kulikuwa na amani kati ya Yabini mfalme wa Hazori na nyumba ya Heberi. 18Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, "Karibu, bwana wangu, karibu kwangu; usiogope." Basi akaingia kwenye hema yake, naye akamfunika kwa nguo.
19Akamwambia, "Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; nina kiu." Akafungua kiriba cha maziwa, akampa anywe, kisha akamfunika tena.
20Akamwambia, "Simama mlangoni pa hema. Mtu akija na kukuuliza, 'Je, kuna mtu hapa?' useme, 'Hapana.'"
21Lakini Yaeli, mke wa Heberi, akatwaa kigingi cha hema na nyundo, akamwendea taratibu, akakipenyeza kile kigingi katika kanieno yake mpaka ardhini, hali amelala usingizi mzito, akiwa amechoka. Hivyo akafa. 22Tazama, Baraka akaja akimfuatia Sisera, naye Yaeli akatoka kumlaki, akamwambia, "Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta." Akaingia pamoja naye, na tazama, Sisera amelala amekufa, kigingi kimepenya katika kanieno yake. 23Siku ile Baba yetu akamtiisha Yabini mfalme wa Kanaani mbele ya Waisraeli. 24Mkono wa Waisraeli ukazidi kumwelemea Yabini mfalme wa Kanaani, hata wakamwangamiza.