Soma. Pokea. Pendekeza.

♥ Maoni

Waamuzi 16

Kitabu

Samsoni Aondoa Malango ya Gaza

Sura ya 16.

Samsoni akaenda Gaza, na huko akamwona kahaba, akaingia kwake. Watu wa Gaza waliposikia, "Samsoni amekuja hapa," wakapazunguka mahali pale, wakimvizia usiku kucha kwenye lango la mji. Wakanyamaza kimya usiku wote, wakisema, "Kutakapopambazuka tutamwua." Samsoni akalala hapo hadi usiku wa manane. Usiku wa manane akaondoka, akakamata milango ya lango la mji na miimo yote miwili, akaing'oa pamoja na komeo lake, akaiweka mabegani mwake, akaipeleka juu ya kilima kinachoelekea Hebroni.

Baada ya haya akampenda mwanamke katika Bonde la Soreki, ambaye jina lake aliitwa Delila. Watawala wa Wafilisti wakamjia, wakamwambia, "Mshawishi upate kujua nguvu zake kuu zapatikana wapi, na jinsi tuwezavyo kumshinda na kumfunga ili kumtiisha. Kila mmoja wetu atakupa vipande 1,100 vya fedha."

Delila akamwambia Samsoni, "Niambie nguvu zako kuu zapatikana wapi, na jinsi ungeweza kufungwa na kutiishwa."

Samsoni akamwambia, "Kama wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, ambazo hazijakauka bado, nitakuwa dhaifu na kuwa kama mtu mwingine yeyote."

Ndipo watawala wa Wafilisti wakamletea kamba saba mbichi za upinde, ambazo hazijakauka bado, naye akamfunga kwazo. Basi alikuwa na watu wakivizia katika chumba cha ndani. Akamwambia, "Wafilisti wanakujia, Samsoni!" Lakini akazikata kamba za upinde kama vile uzi wa kitani ukatikavyo uugusapo moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikugunduliwa.

Delila akamwambia Samsoni, "Umenidhihaki na kuniambia uongo. Sasa niambie jinsi unavyoweza kufungwa."

Akamwambia, "Kama wakinifunga vizuri kwa kamba mpya ambazo hazijatumika kamwe, nitakuwa dhaifu, kama mtu mwingine yeyote."

Delila akachukua kamba mpya akamfunga kwazo, akisema, "Samsoni, Wafilisti wanakujia!" Watu walikuwa wakivizia katika chumba cha ndani. Lakini akazikata kamba mikononi mwake kama uzi.

Delila akamwambia Samsoni, "Umenidhihaki na kuniambia uongo wakati wote huu. Niambie jinsi unavyoweza kufungwa." Akamwambia, "Ukifuma zile shungi saba za kichwa changu katika nguo ya kitanda cha kufumia na kuikaza kwa msumari, nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote."

Akaikaza kwa msumari, akamwambia, "Samsoni, Wafilisti wanakujia!" Lakini akaamka usingizini akaung'oa msumari, na kitanda cha kufumia, na ile nguo.

Akamwambia, "Wawezaje kusema 'Nakupenda' hali moyo wako hauko pamoja nami? Mara tatu umenidhihaki wala hukuniambia nguvu zako kuu zapatikana wapi."

Basi alipomsonga kwa maneno yake siku baada ya siku na kumhimiza sana, akachoka nafsi yake hata akatamani kufa. Basi akamwambia moyo wake wote: "Wembe haujawahi kugusa kichwa changu, kwa maana mimi ni Mnadhiri wa Baba yetu tangu tumbo la mama yangu. Nikinyolewa, nguvu zangu zitaniondoka, nami nitakuwa dhaifu, kama mtu mwingine yeyote."

Delila alipoona amemwambia moyo wake wote, akatuma kuwaita watawala wa Wafilisti, akisema: "Njooni tena mara hii moja, kwa maana ameniambia moyo wake wote." Basi wakamjia wakiwa na ile fedha mikononi mwao. Akamlaza usingizi magotini pake, akamwita mtu, akamnyoa zile shungi saba za kichwa chake. Akaanza kumtiisha, nazo nguvu zake zikamwondoka. Akasema, "Wafilisti wanakujia, Samsoni!" Akaamka usingizini akawaza, "Nitatoka kama mara nyingine na kujikung'uta niwe huru." Lakini hakujua ya kuwa Baba yetu amemwacha.

Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho, wakamleta Gaza. Wakamfunga kwa pingu za shaba, naye akawa akisaga nafaka gerezani. Lakini nywele za kichwa chake zikaanza kuota tena baada ya kunyolewa.

Baba Amtia Nguvu Samsoni Tena

Watawala wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea Dagoni mungu wao dhabihu kuu na kufurahi, wakisema, "Mungu wetu amemtia Samsoni adui yetu mikononi mwetu." Watu walipomwona, wakamsifu mungu wao, wakisema, "Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu, aliyeharibu nchi yetu na kuongeza waliouawa wetu."

Mioyo yao ilipokuwa na furaha, wakasema, "Mwiteni Samsoni ili atuchezee." Basi wakamleta Samsoni kutoka gerezani, naye akawachezea. Wakamsimamisha kati ya nguzo. Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, "Niache nizishike nguzo ambazo nyumba imekaa juu yake, ili niweze kuzitegemea." Ile nyumba ilikuwa imejaa wanaume na wanawake; watawala wote wa Wafilisti walikuwako, na juu ya paa walikuwako wanaume na wanawake wapatao 3,000 wakimtazama Samsoni akicheza. Ndipo Samsoni akamwita Baba yetu: "Ee Baba Mwenye Enzi, unikumbuke, nakuomba. Unitie nguvu mara hii moja tu, ili kwa pigo moja niwalipize Wafilisti haki kwa ajili ya macho yangu mawili." Samsoni akazishika zile nguzo mbili za katikati zilizoishikilia nyumba, akazitegemea, mkono wake wa kuume juu ya moja, na wa kushoto juu ya nyingine. Samsoni akasema, "Na nife pamoja na Wafilisti." Akasukuma kwa nguvu zake zote, nayo nyumba ikawaangukia watawala na watu wote waliokuwamo ndani yake. Hivyo akaua watu wengi zaidi katika kufa kwake kuliko katika uhai wake.

Ndugu zake na jamaa yote ya baba yake wakashuka, wakamchukua, wakampandisha, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli katika kaburi la Manoa baba yake. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka ishirini.

A young man reading the Father's Heart Bible print edition in a coffee shop Sasa Imechapishwa

Maoni

Mawazo, maswali, au neno ambalo sura hii imeliamsha ndani yako — lishiriki hapa. Kila maoni huweka jina lako kwenye Wall of Contributors.

Kusoma, kunakili na kushiriki ni wazi kwa kila mtu — huhitaji akaunti. Kutoa maoni, kutia alama, na kuhifadhi mahali ulipofikia hupatikana kwa akaunti ya bure, na kila maoni huweka jina lako kwenye Wall of Contributors.

Jiunge na Familia — ni bure →
  • Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kuchangia.