Baba Awafanya Upya Watu Wake huko Gilgali
5 1Ikawa wafalme wote wa Waamori waliokuwa upande wa magharibi wa Yordani, na wafalme wote wa Wakanaani waliokuwa kando ya bahari, waliposikia ya kwamba Baba yetu ameyakausha maji ya Yordani mbele ya Israeli hata wakavuka, mioyo yao ikayeyuka, wala haikubaki roho ndani yao kwa sababu ya wana wa Israeli.
2Wakati ule Baba yetu akamwambia Yoshua, "Jifanyie visu vya mawe, ukawatahiri wana wa Israeli tena mara ya pili."
3Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe, akawatahiri wana wa Israeli hapo Gibeath-haaralothi, yaani Kilima cha Magovi. 4Na sababu ya Yoshua kuwatahiri ndiyo hii: watu wote waliotoka Misri, yaani wanaume, watu wote wa vita, walikuwa wamekufa jangwani njiani, walipokwisha kutoka Misri. 5Kwa maana watu wote waliotoka walikuwa wametahiriwa, bali watu wote waliozaliwa jangwani njiani walipotoka Misri hawakuwa wametahiriwa. 6Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea miaka arobaini jangwani, hata taifa lote, watu wa vita waliotoka Misri, walipokwisha kuangamia, kwa sababu hawakuitii sauti ya Baba yetu; ambao Baba yetu aliwaapia ya kwamba hatawaacha waione nchi ile aliyowaapia baba zao kutupa sisi, nchi ijaayo maziwa na asali. 7Naye akawainua watoto wao mahali pao, nao ndio Yoshua aliowatahiri; kwa maana walikuwa hawajatahiriwa, kwa sababu hawakuwa wametahiriwa njiani. 8Ikawa walipokwisha kutahiriwa taifa lote, walikaa mahali pao kambini hata walipopona.
9Kisha Baba yetu akamwambia Yoshua, "Leo nimeivingirisha aibu ya Misri iondoke kwenu." Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Gilgali hata leo.
10Wana wa Israeli wakapiga kambi huko Gilgali; wakaifanya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. 11Wakala mazao ya nchi siku ya pili baada ya Pasaka, siku iyo hiyo, mikate isiyotiwa chachu, na bisi. 12Ile mana ikakoma siku ya pili baada ya kula mazao ya nchi; wana wa Israeli hawakuwa na mana tena, bali wakala matunda ya nchi ya Kanaani mwaka ule.
Jemadari wa Jeshi la Baba
13Ikawa Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho yake akaona, na tazama, mtu amesimama mbele yake, na upanga wake mkononi mwake umefutwa alani. Yoshua akamwendea, akamwuliza, "Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu?"
14Akasema, "La; bali nimekuja sasa nikiwa jemadari wa jeshi la Baba yetu." Yoshua akaanguka kifudifudi hata nchi, akasujudu, akamwambia, "Bwana wangu ana neno gani kwa mtumishi wake?"
15Yule jemadari wa jeshi la Baba yetu akamwambia Yoshua, "Vua viatu vyako miguuni mwako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu." Yoshua akafanya vivyo.