Baba Anatoa Miji ya Makimbilio
20 1Kisha Baba yetu akamwambia Yoshua:
2"Waambie Waisraeli: 'Jichagulieni miji ya makimbilio niliyowaambia kwa mkono wa Musa, 3ili kila auaye mtu kwa bahati mbaya, pasipo kujua, aweze kukimbilia huko—makimbilio kwenu dhidi ya mlipiza kisasi cha damu. 4Kila akimbiliaye mmojawapo wa miji hii atasimama penye ingilio la lango la mji na kutoa habari zake mbele ya wazee wa mji ule. Nao watamkaribisha ndani ya mji, watampa mahali, na kumwacha akae kati yao. 5Kama mlipiza kisasi cha damu akimfuatia, kamwe wasimtoe muuaji mikononi mwake, kwa sababu alimpiga jirani yake pasipo kujua, wala hakuwa na chuki naye tangu awali. 6Ni lazima akae katika mji ule mpaka atakaposimama kuhukumiwa mbele ya mkutano, na mpaka atakapokufa kuhani mkuu atumikaye wakati ule. Kisha muuaji aweza kurudi katika mji wake mwenyewe na nyumbani kwake, mji ule aliokimbia.'"
7Kwa hiyo wakatenga Kedeshi katika Galilaya, vilimani mwa Naftali; Shekemu, vilimani mwa Efraimu; na Kiriath-arba (yaani Hebroni), vilimani mwa Yuda. 8Ng'ambo ya Yordani, upande wa mashariki wa Yeriko, wakatoa Bezeri katika nyika iliyoko juu ya uwanda wa juu kutoka kabila la Reubeni, Ramothi katika Gileadi kutoka kabila la Gadi, na Golani katika Bashani kutoka kabila la Manase. 9Hii ndiyo miji iliyochaguliwa kwa ajili ya Waisraeli wote na wageni wakaao kati yao, ili kila auaye mtu bila kusudi aweze kukimbilia huko na asife kwa mkono wa mlipiza kisasi cha damu kabla ya kusimama kuhukumiwa mbele ya mkutano.