Siku Zangu ni Pumzi Tu
7 1"Je, wanadamu hawana utumishi mgumu duniani, wala siku zao si kama zile za mtu wa kuajiriwa? 2Kama mtumwa anayetamani kivuli, na kama mtu wa kuajiriwa angojaye mshahara wake, 3vivyo hivyo nimegawiwa miezi ya ubatili, na usiku wa taabu nimepangiwa. 4Nilalapo nasema, 'Nitaondoka lini?' Lakini usiku hujikokota, nami najigeuzageuza hata mapambazuko. 5Mwili wangu umevikwa funza na mabonge ya udongo; ngozi yangu hukauka, kisha hupasuka tena. 6Siku zangu ni za haraka kuliko chombo cha mfumaji, nazo zinafika mwisho wake bila tumaini. 7Kumbuka ya kuwa maisha yangu ni pumzi tu; sitaona tena jambo lolote jema. 8Jicho linaloniona sasa halitaniona tena; macho yako yatakuwa juu yangu, nami sitakuwapo. 9Kama wingu linavyofifia na kutoweka, ndivyo yeye ashukaye kaburini asivyopanda tena; 10harudi tena nyumbani mwake, wala mahali pake hapamjui tena.
11"Kwa hiyo sitanyamazisha kinywa changu; nitanena katika dhiki ya roho yangu, nitalalamika katika uchungu wa nafsi yangu. 12Je, mimi ni bahari, au nyoka wa baharini, hata umeniwekea ulinzi? 13Nisemapo, 'Kitanda changu kitanifariji, malazi yangu yatapunguza malalamiko yangu,' 14ndipo unaponitisha kwa ndoto na kuniogofya kwa maono, 15hata ningechagua kunyongwa na kufa kuliko mwili wangu huu. 16Nachakaa; sitaishi milele. Niache, kwa maana siku zangu ni pumzi.
17"Mwanadamu ni kitu gani, hata umtukuze hivyo, na kumkazia moyo wako, 18hata ukamjilie kila asubuhi na kumjaribu kila dakika? 19Hata lini utaacha kuniangalia mbali nami, na kuniacha peke yangu muda wa kutosha kumeza mate yangu? 20Kama nimefanya dhambi, nimekutenda nini wewe, Ee mlinzi wa wanadamu? Mbona umenifanya kuwa shabaha yako, hata nimekuwa mzigo kwa nafsi yangu mwenyewe? 21Mbona hutaki kunisamehe dhambi yangu na kuniondolea uovu wangu? Kwa maana karibu nitalala mavumbini; utanitafuta, lakini sitakuwapo."