Maneno ya Kusema kwa Niaba ya Mungu
36 1Kisha Elihu akaendelea, akasema: 2"Nivumilie kidogo, nami nitakuonyesha, kwa maana bado kuna maneno ya kusema kwa niaba ya Mungu. 3Nitayaleta maarifa yangu kutoka mbali, nami nitampa Muumba wangu haki. 4Kwa kweli maneno yangu si ya uongo; mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja nawe. 5Tazama, Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mtu; ni mwenye nguvu katika uweza wa ufahamu. 6Hawahifadhi waovu hai, bali huwapa haki wateswao. 7Hawaondoi kamwe macho yake kwa wenye haki; huwaketisha pamoja na wafalme katika viti vyao vya enzi milele, nao hutukuzwa. 8Nao ikiwa wamefungwa kwa minyororo, wamenaswa katika kamba za mateso, 9ndipo huwaonyesha matendo yao na maasi yao, kwamba wamejivuna kwa kiburi. 10Huufungua masikio yao ili wapate mafunzo, na kuamuru kwamba wageuke kutoka dhambini. 11Kama wakisikia na kumtumikia, huzimaliza siku zao katika kufanikiwa, na miaka yao hupita kwa furaha. 12Lakini kama hawasikii, huangamia kwa upanga, na kufa bila maarifa. 13Wasiomcha Mungu mioyoni mwao huweka ghadhabu; hawalii kuomba msaada anapowafunga. 14Nafsi yao hufa katika ujana, na maisha yao huishia miongoni mwa makahaba wa mahali pa ibada. 15Huwaokoa wateswao kwa njia ya mateso yao, na kuyafungua masikio yao kwa dhiki. 16Naye angekutoa pia katika makucha ya dhiki hadi mahali panapoenea, palipo wazi pasipo kizuizi, na meza yako ingeandaliwa kwa unono. 17Lakini umejawa na hukumu inayowastahili waovu; hukumu na haki vimekushika. 18Jihadhari isije ghadhabu ikakushawishi kudhihaki, wala usiache fidia kubwa ikupotoshe. 19Je, kilio chako cha kuomba msaada kitakuepusha na dhiki, au nguvu zako zote? 20Usiutamani usiku, ambapo mataifa hukatiliwa mbali kutoka mahali pao. 21Jihadhari; usigeukie dhambi, kwa maana umependelea hii kuliko mateso. 22Tazama, Mungu ametukuzwa katika uweza wake; ni nani aliye mwalimu kama yeye?
23"Ni nani aliyemwagizia njia yake, au ni nani awezaye kusema, 'Umetenda vibaya'? 24Kumbuka kuyaadhimisha matendo yake, ambayo watu wameyaimba kwa nyimbo. 25Wanadamu wote wameyatazama; binadamu huyaona kutoka mbali. 26Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui; hesabu ya miaka yake haitafutiki. 27Kwa maana huvuta matone ya maji; huchujwa kama mvua kutoka ukungu wake, 28ambayo mawingu huyamwaga na kuyadondosha kwa wingi juu ya wanadamu. 29Je, kuna mtu awezaye kuelewa kutandazwa kwa mawingu, ngurumo ya hema yake? 30Tazama, hueneza umeme wake kumzunguka, na kuvifunika vilindi vya bahari. 31Kwa maana kwa hivi huwatawala mataifa; hutoa chakula kwa wingi. 32Huzijaza mikono yake kwa umeme, na kuuamuru upige shabaha. 33Ngurumo yake humtangaza; hata mifugo huhisi dhoruba inavyokuja."