Rafiki Zake Ayubu Wanyamaza
32 1Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa sababu alikuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe. 2Ndipo hasira ya Elihu, mwana wa Barakeli, Mbuzi, wa jamaa ya Ramu, ikawaka sana. Hasira yake ikawaka juu ya Ayubu kwa sababu alijihesabia haki mwenyewe kuliko Mungu. 3Pia hasira yake ikawaka juu ya rafiki zake Ayubu watatu, kwa sababu hawakupata jibu, na hata hivyo walikuwa wamemhukumu Ayubu. 4Basi Elihu alikuwa amesubiri kusema na Ayubu kwa sababu wale wengine walikuwa wazee kuliko yeye. 5Lakini Elihu alipoona kwamba watu hawa watatu hawakuwa na neno la kusema, hasira yake ikawaka. 6Basi Elihu, mwana wa Barakeli, Mbuzi, akanena akasema: "Mimi ni mchanga wa miaka, nanyi ni wazee; kwa hiyo nilijizuia, nikiogopa kuwaambia niyajuayo. 7Nikafikiri, 'Umri na useme, na wingi wa miaka ufundishe hekima.' 8Lakini ni roho iliyomo ndani ya mtu, pumzi ya Mwenyezi, ndiyo itiayo ufahamu. 9Si wazee ndio wenye hekima, wala si wenye umri mkubwa ndio wafahamuo lililo haki. 10Kwa hiyo nasema, nisikilizeni; mimi nami nitasema niyajuayo. 11Tazameni, nilingoja maneno yenu; nilisikiliza hoja zenu mlipokuwa mkitafuta la kusema. 12Niliwatega masikio kwa makini; lakini hakuna hata mmoja wenu aliyemthibitisha Ayubu kuwa amekosea au kuzijibu hoja zake. 13Basi msiseme, 'Tumeipata hekima; Mungu na amshinde, wala si mwanadamu.' 14Ayubu hakuyapanga maneno yake kunielekea mimi, wala sitamjibu kwa hoja zenu. 15Wamefadhaika, hawana la kusema tena; maneno yamewaishia. 16Je, nisubiri, sasa wamenyamaza, sasa wamesimama pale bila jibu? 17Mimi nami nitatoa hoja yangu; mimi nami nitasema niyajuayo. 18Kwa maana nimejaa maneno; roho iliyomo ndani yangu inanisukuma. 19Ndani yangu ni kama divai isiyo na tundu la kupumua, kama viriba vipya vilivyo tayari kupasuka. 20Sharti niseme ili nipate afueni; sharti nifumbue midomo yangu nijibu. 21Sitampendelea mtu ye yote, wala sitambembeleza mtu ye yote; 22kwa maana sijui kubembeleza—kama ningejua, Muumba wangu angeniondoa upesi."