Ayubu Apaza Sauti Yake Tena
27 1Ayubu akaendelea tena na hotuba yake, akasema: 2"Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu, na Mwenyezi, aliyeitia uchungu nafsi yangu, 3maadamu pumzi yangu ingalimo ndani yangu, na roho wa Baba yetu ingali puani mwangu, 4midomo yangu haitanena uongo, wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu. 5Sitakubali kamwe ya kuwa mna haki; hata nife sitauacha uadilifu wangu. 6Naishika sana haki yangu, wala sitaiacha; moyo wangu haunilaumu kwa siku zangu zozote.
7"Adui yangu na awe kama mwovu, na yeye ainukaye juu yangu na awe kama asiye na haki. 8Kwa maana tumaini la asiyemcha Mungu ni nini akatiliwapo mbali, Mungu aitwaapo nafsi yake? 9Je! Mungu atailisikia kilio chake dhiki impatapo? 10Je! Atajifurahisha katika Mwenyezi? Je! Atamwita Mungu kila wakati? 11Nitawafundisha habari za mkono wa Mungu; sitayaficha yaliyoko kwa Mwenyezi. 12Tazameni, ninyi nyote mmeyaona haya wenyewe; mbona basi mnanena maneno matupu hivyo? 13Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kutoka kwa Mungu, urithi wapokeao wadhalimu kutoka kwa Mwenyezi: 14Watoto wake wakiwa wengi, wataanguka kwa upanga, na wazao wake hawatashiba mkate. 15Wale wake watakaosalia baada yake watazikwa kwa tauni, na wajane wao hawatalia. 16Ajapokusanya fedha kama mavumbi, na kurundika mavazi kama udongo, 17aweza kuyarundika, lakini mwenye haki atayavaa, na asiye na hatia atazigawa fedha. 18Ajenga nyumba yake kama kifukofuko cha nondo, kama kibanda achukicho mngoja-zamu. 19Hulala akiwa tajiri, lakini hatafanya hivyo tena; hufumbua macho yake, na hayako. 20Vitisho humpata kama gharika; wakati wa usiku kisulisuli humwondoa. 21Upepo wa mashariki humwinua, naye huenda zake; humfagilia mbali na mahali pake. 22Humrukia bila kumhurumia; hukimbia kwa kasi mbele ya nguvu zake. 23Huwapigia makofi, na kumzomea atoke mahali pake."