Ayubu Ajibu
26 1Ndipo Ayubu akajibu: 2"Jinsi ulivyomsaidia asiye na nguvu! Jinsi ulivyouokoa mkono usio na uwezo! 3Jinsi ulivyomshauri asiye na hekima, na kumkirimia ufahamu mzuri kwa wingi! 4Kwa msaada wa nani umenena maneno haya? Na pumzi ya nani ilitoka kwako? 5Roho zilizoondoka hutetemeka—wale walio chini ya maji na wote wakaao humo. 6Kaburi liko wazi mbele za Baba yetu, na Uharibifu hauna kifuniko. 7Yeye huzitandaza mbingu za kaskazini juu ya nafasi tupu; huiangika dunia juu ya utupu. 8Huyafunga maji katika mawingu yake mazito, wala mawingu hayapasuki chini ya uzito wake. 9Huufunika uso wa mwezi mpevu, akiyatandaza mawingu yake juu yake. 10Amechora mviringo juu ya uso wa maji, penye mpaka kati ya nuru na giza. 11Nguzo za mbingu hutetemeka, zikishangaa kwa kukemea kwake. 12Kwa nguvu zake aliituliza bahari; kwa ufahamu wake alimponda yule joka la baharini Rahabu. 13Kwa pumzi yake mbingu zilikuwa angavu; mkono wake alimchoma yule nyoka akimbiaye. 14Na haya ni pambizo tu za njia zake—jinsi ilivyo hafifu minong'ono tunayoisikia juu yake! Lakini ngurumo ya nguvu zake, ni nani awezaye kuielewa?"