Ayubu Ajibu: Kwa Nini Waovu Hufanikiwa?
21 1Ndipo Ayubu akajibu: 2"Sikilizeni kwa makini maneno yangu, na hii iwe faraja mnayonipa. 3Nivumilieni ninaposema, na baada ya kusema, mwaweza kuendelea kudhihaki. 4Nami je, lalamiko langu ni juu ya mwanadamu tu? Kwa nini nisikose subira? 5Nitazameni na kushangaa, na kuweka mkono wenu kinywani mwenu. 6Ninapokumbuka jambo hili, naogopa, na kutetemeka kunaushika mwili wangu. 7Kwa nini waovu huendelea kuishi, wakizeeka na kuongezeka nguvu? 8Watoto wao wamethibitika na wako salama pamoja nao mbele ya macho yao, na wazao wao mbele ya kuona kwao. 9Nyumba zao ni salama na hazina hofu, wala fimbo ya Mungu haiwaangukii. 10Fahali wao huzalisha wala hakosi kamwe; ng'ombe wao huzaa wala hana mimba iliyoharibika. 11Huwaacha wadogo wao wakimbie huru kama kundi, na watoto wao hurukaruka. 12Huimba kwa matari na kinubi, na kufurahi kwa sauti ya filimbi. 13Hutumia siku zao katika ufanisi, na kwa amani hushuka kaburini. 14Lakini humwambia Mungu, 'Tuache! Hatuna hamu ya kuzijua njia zako. 15Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutapata faida gani kwa kumwomba?' 16Lakini ufanisi wao hauko mikononi mwao wenyewe; sitaki kitu chochote na shauri la waovu. 17Ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa? Ni mara ngapi maafa yao huwaangukia? Ni mara ngapi Mungu hugawa maumivu katika hasira yake? 18Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo, kama makapi ambayo dhoruba huyapeperusha? 19Mnasema, 'Mungu huweka akiba ya adhabu ya mtu kwa ajili ya watoto wake.' Na amlipe mtu mwenyewe, ili aijue. 20Macho yake mwenyewe na yaone uangamivu wake, naye anywe ghadhabu ya Mwenyezi. 21Kwa maana anajali nini juu ya nyumba yake baada yake, hesabu ya miezi yake ikikatwa? 22Je, kuna yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa, ikiwa yeye ndiye anayewahukumu walio juu? 23Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu kamili, akiwa katika starehe kabisa na salama, 24mwili wake ukiwa umenawiri vizuri na uboho wa mifupa yake ungali unyevunyevu. 25Mwingine hufa akiwa na nafsi yenye uchungu, bila kamwe kuonja jema lolote. 26Kwa pamoja hulala mavumbini, na funza huwafunika wote wawili. 27Tazameni, ninayajua mawazo yenu, na hila zenu za kunitenda mabaya. 28Kwa maana mnasema, 'Iko wapi sasa nyumba ya mtu mkuu? Iko wapi hema ambapo waovu walikaa?' 29Je, hamjawahi kuwauliza wale wasafirio barabarani? Hamtakubali ushahidi wanaotoa, 30kwamba mtu mwovu huepushwa katika siku ya maafa, kwamba huokolewa katika siku ya ghadhabu? 31Ni nani anayemkabili uso kwa uso kwa ajili ya mwenendo wake, na ni nani anayemlipa kwa yale aliyoyatenda? 32Hubebwa hadi kaburini, na ulinzi huwekwa juu ya kaburi lake. 33Udongo wa bondeni ni mtamu kwake; kila mtu humfuata nyuma yake, na wale waliomtangulia hawana hesabu. 34Basi mwawezaje kunifariji kwa maneno matupu? Majibu yenu si kitu ila uongo tu."