Wafariji Wenye Kuudhi
16 1Ndipo Ayubu akajibu: 2"Nimeyasikia mambo mengi kama haya; ninyi nyote ni wafariji wenye kuudhi. 3Je, hakuna mwisho wa maneno yenu yasiyo na maana? Ni nini kinachokuchokoza hata uendelee kujibu? 4Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi, kama ninyi mngekuwa mahali pangu; ningeweza kufungamanisha maneno dhidi yenu na kuwatikisia kichwa changu. 5Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, na faraja ya midomo yangu ingepunguza maumivu yenu. 6Ninaponena, maumivu yangu hayapunguki; nami ninaponyamaza, ni nini kinachoniondokea? 7Hakika sasa Mungu amenichosha; umeliharibu kabisa kundi langu lote. 8Umeninyausha, na jambo hilo limekuwa shahidi; ukonde wangu unainuka juu yangu na kunishuhudia usoni pangu. 9Hasira yake imenirarua na kunishambulia; amenisagia meno yake; adui yangu ananikazia macho yake. 10Watu wamenifumbulia vinywa vyao; wamenipiga shavu kwa dharau; wanashikamana pamoja dhidi yangu. 11Mungu ananitia mikononi mwa wasio na haki na kunitupa katika mtego wa waovu. 12Nilikuwa na raha, naye akanivunja vunja; alinishika shingoni na kunipasua vipande vipande; amenisimamisha niwe shabaha yake. 13Wapiga mishale wake wamenizunguka; anazipasua figo zangu bila huruma na kuimwaga nyongo yangu chini. 14Ananivunja kwa pigo baada ya pigo; ananishambulia kama shujaa wa vita. 15Nimeshona nguo za maombolezo juu ya ngozi yangu, na kuuzika uso wangu mavumbini. 16Uso wangu umewekwa wekundu kwa kulia, na kivuli kizito kimekaa juu ya kope zangu, 17ingawa hakuna dhuluma mikononi mwangu, na maombi yangu ni safi. 18Ee nchi, usiifunike damu yangu, na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika. 19Hata sasa, shahidi wangu yuko mbinguni, na mtetezi wangu yuko juu. 20Rafiki zangu wananidharau; jicho langu linamwagia Mungu machozi, 21ili atetee shauri la mtu mbele za Mungu, kama mwana wa Adamu anavyomtetea jirani yake. 22Kwa maana miaka michache tu itapita, kisha nitaiendea njia ile isiyo na kurudi."