Sofari Ajibu
11 1Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu: 2"Je, mafuriko haya ya maneno yasijibiwe? Je, mtu aliyejaa maneno hivyo athibitishwe kuwa yu sahihi? 3Je, maneno yako matupu yawanyamazishe wengine? Je, utadhihaki bila mtu wa kukutia aibu? 4Kwa maana wasema, 'Mafundisho yangu ni safi, nami ni safi machoni pako.' 5Lakini laiti, kama Mungu angesema tu na kufungua midomo yake dhidi yako, 6na kukufunulia siri za hekima—kwa maana hekima ya kweli ina pande mbili. Basi ujue ya kuwa Mungu amekutoza kidogo kuliko hatia yako inavyostahili. 7Je, waweza kuvumbua mambo ya ndani ya Mungu? Je, waweza kuupata mpaka wa Mwenyezi? 8Ni ya juu kuliko mbingu—waweza kufanya nini? Ni ya kina kuliko kaburi—waweza kujua nini? 9Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia na kipana kuliko bahari. 10Kama akipita na kufunga gerezani na kuita hukumuni, ni nani awezaye kumzuia? 11Kwa maana yeye huwajua watu wasiofaa; aonapo uovu, je, hatauangalia? 12Lakini mtu mpumbavu atapata hekima punda-mwitu atakapozaa mtoto wa kibinadamu. 13Kama ukiutengeneza moyo wako na kuinyoosha mikono yako kumwelekea, 14kama dhambi imo mkononi mwako, iondoe, wala usiache udhalimu ukae hemani mwako, 15ndipo hakika utauinua uso wako, bila aibu; utasimama imara wala hutaogopa. 16Utaisahau taabu yako, ukiikumbuka kama maji yaliyokwisha kupita. 17Maisha yako yatang'aa kuliko adhuhuri; giza lake litakuwa kama asubuhi. 18Utakuwa salama, kwa sababu kuna tumaini; utatazama pande zote na kulala salama. 19Utalala bila mtu wa kukuogofya, na wengi watajipendekeza kwako. 20Lakini macho ya waovu yatazimia; kila njia ya kuponyokea itawapotea, na tumaini lao pekee ni kutoa pumzi yao ya mwisho."