Abrahamu huko Gerari
20 1Abrahamu akasafiri kutoka huko kuelekea Negebu, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akaishi kama mgeni huko Gerari. 2Abrahamu akasema juu ya Sara, mkewe, "Yeye ni dada yangu." Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma watu, akamchukua Sara.
3Lakini Baba yetu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku ule: "Wewe ni kama mfu kwa sababu ya mwanamke uliyemchukua, kwa maana ni mke wa mtu."
4Lakini Abimeleki alikuwa hajamkaribia. Akasema, "Bwana Mungu, je, utaliangamiza hata taifa lisilo na hatia? 5Je, yeye mwenyewe hakuniambia, 'Ni dada yangu'? Naye mwenyewe pia alisema, 'Ni kaka yangu.' Nimefanya jambo hili kwa moyo mnyofu na kwa mikono isiyo na hatia."
6Ndipo Baba yetu akamwambia katika ndoto, "Naam, ninajua kwamba umefanya jambo hili kwa unyofu wa moyo, nami nimekuzuia usinitende dhambi mimi—ndiyo maana sikukuacha umguse. 7Sasa mrudishie mtu huyo mke wake, kwa maana yeye ni nabii atakayekuombea, nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwamba hakika utakufa, wewe na wote ulio nao."
8Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumishi wake wote, akawaambia mambo haya yote; watu wale wakaogopa sana. 9Abimeleki akamwita Abrahamu, akamuuliza, "Umetutenda nini? Nimekukosea nini, hata ukaniletea mimi na ufalme wangu dhambi kubwa kiasi hiki? Umenitendea mambo ambayo hayakupasa kutendeka." 10Abimeleki akamwambia tena Abrahamu, "Ulikuwa unawaza nini, hata ukafanya jambo kama hili?"
11Abrahamu akasema, "Nilifikiri: hakika hapa hakuna hofu ya Baba yetu, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu." 12Zaidi ya hayo, kweli yeye ni dada yangu, binti wa baba yangu ingawa si wa mama yangu, naye akawa mke wangu.
13Baba yetu aliponifanya nitangetange mbali na nyumba ya baba yangu, nilimwambia: Nifanyie wema huu—kila mahali tuendako, sema juu yangu, "Yeye ni kaka yangu."
14Abimeleki akachukua kondoo, ng'ombe, na watumishi wa kiume na wa kike, akampa Abrahamu, akamrudishia Sara mkewe. 15Abimeleki akasema, "Nchi yangu iko wazi mbele yako; kaa mahali popote upendapo." 16Naye akamwambia Sara, "Tazama, ninampa ndugu yako vipande 1,000 vya fedha. Hii ni kufunika kosa ulilotendewa mbele ya macho ya wote walio pamoja nawe; mbele ya kila mtu umetakaswa kabisa."
17Abrahamu akamwomba Baba yetu, naye akamponya Abimeleki, mkewe, na watumishi wake wa kike, hata wakaweza kuzaa tena, 18kwa maana Baba yetu alikuwa amefunga kabisa kila tumbo katika nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.