Baba Aihukumu Tiro
Tiro anafaidika na maangamizi ya Yerusalemu, akitazamia biashara zaidi sasa kwa kuwa lango limevunjika. Baba yetu asema mataifa yatakuja juu yake kama mawimbi. Nebukadneza atazibomoa kuta zake, mawe yake yatatupwa baharini, na mahali pake pataachwa jabali tupu pa kutandaza nyavu.
26 1Katika mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Baba yetu likanijia, kusema:
2Mwanadamu, kwa sababu Tiro ameinena juu ya Yerusalemu, akisema, 'Aha! Lango la mataifa limevunjika; limefunguliwa kwangu. Yeye amelala magofu; nami nitatajirika.' 3Kwa sababu hiyo Bwana Baba asema hivi: Tazama, mimi ni juu yako, Tiro. Nitaleta mataifa mengi juu yako, kama bahari iinuavyo mawimbi yake. 4Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; nami nitauondoa udongo wake, na kumwacha awe jabali tupu. 5Atakuwa mahali pa kutandaza nyavu katikati ya bahari; kwa maana mimi nimenena, asema Bwana Baba; naye atakuwa mateka kwa mataifa, 6na vijiji vyake vilivyo bara vitauawa kwa upanga. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi Baba.
7Bwana Baba asema hivi: Tazama, nitamleta Nebukadneza mfalme wa Babeli, mfalme wa wafalme, juu ya Tiro kutoka kaskazini, pamoja na farasi, na magari, na wapanda farasi, na kusanyiko kubwa la watu wengi. 8Atawaua vijiji vyako vilivyo bara kwa upanga; naye atajenga boma juu yako, na kufanya chuguu juu yako, na kuinua ngao juu yako. 9Naye atazipiga kuta zako kwa vyombo vyake vya kubomolea, na kuibomoa minara yako kwa mashoka yake. 10Farasi wake ni wengi, hata mavumbi yao yatakufunika; kuta zako zitatetemeka kwa mshindo wa wapanda farasi, na magurudumu, na magari, atakapoingia malangoni mwako, kama watu waingiavyo mji ambao kuta zake zimebomolewa. 11Kwa kwato za farasi wake atazikanyaga njia zako zote; atawaua watu wako kwa upanga, na nguzo zako zenye nguvu zitaanguka chini. 12Watateka mali zako, na kuipora bidhaa yako, na kuzibomoa kuta zako, na kuziharibu nyumba zako nzuri; nao watatupa mawe yako, na miti yako, na kifusi chako katikati ya bahari. 13Nami nitaikomesha sauti ya nyimbo zako; wala sauti ya vinubi vyako haitasikika tena. 14Nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa kutandaza nyavu; hutajengwa tena kamwe; kwa maana mimi, Baba, nimenena, asema Bwana Baba.
15Bwana Baba amwambia Tiro hivi: Je! Visiwa havitatetemeka kwa mshindo wa kuanguka kwako, wakati majeruhi wanapougua, wakati machinjo yatakapokuwa katikati yako? 16Ndipo wakuu wote wa bahari watashuka kutoka viti vyao vya enzi, na kuyavua majoho yao, na kuyavua mavazi yao yaliyotariziwa; watajivika kutetemeka; wataketi chini, wakitetemeka kila dakika, na kukustaajabia. 17Nao watakuombolezea, wakikuambia, 'Jinsi ulivyoangamia, ewe mji uliyesifiwa, uliyekaliwa na watu waliotoka baharini, uliyekuwa hodari juu ya bahari, wewe na wenyeji wako, waliowatia hofu wote waliokaa humo!' a a v17 Tiro ulikuwa mji-dola wa kisiwani wenye utajiri, ambao nguvu zake na wingi wa watu wake vilijengwa juu ya biashara ya baharini. 18Sasa visiwa vinatetemeka katika siku ya kuanguka kwako; naam, visiwa vilivyomo baharini vinafadhaika kwa kuondoka kwako.
19Bwana Baba asema hivi: Nitakapokufanya kuwa mji ukiwa, kama miji isiyokaliwa na watu; nitakapovipandisha vilindi juu yako, na maji makuu yatakapokufunika, 20ndipo nitakapokushusha pamoja na hao washukao shimoni, kwa watu wa zamani za kale; nami nitakukalisha katika nchi za chini, katika mahame ya kale, pamoja na hao washukao shimoni, ili usirudi, wala usijipatie mahali katika nchi ya walio hai. 21Nitakuletea uharibifu wa kutisha, wala hutakuwapo tena; ijapokuwa utatafutwa, hutaonekana tena milele, asema Bwana Baba.