Musa na Haruni Mbele ya Farao
5 1Baadaye Musa na Haruni wakaenda kwa Farao na kusema, "Baba yetu wa Israeli asema hivi: Waache watu wangu waende ili wanifanyie sikukuu jangwani."
2Farao akasema, "Mungu ni nani, hata niitii sauti yake na kuwaacha Israeli waende? Simjui Mungu, wala sitawaacha Israeli waende."
3Wakasema, "Baba yetu amekutana nasi. Turuhusu twende safari ya siku tatu jangwani ili tumtolee Baba yetu dhabihu, asije akatupiga kwa tauni au upanga."
4Lakini mfalme wa Misri akawaambia, "Musa na Haruni, kwa nini mnawavuta watu waache kazi zao? Rudini kazini kwenu!" 5Farao akasema, "Tazama, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnataka wakome kufanya kazi!"
6Siku iyo hiyo Farao akawaamuru wasimamizi wa watumwa na wanyapara juu ya watu, akisema: 7"Msiendelee kuwapa watu majani ya kutengeneza matofali kama zamani. Waende wenyewe wakakusanye majani.
8Lakini watakieni kiasi kile kile cha matofali kama zamani; msipunguze. Wao ni wavivu; ndiyo maana wanalia, 'Turuhusu twende tukamtolee Mungu wetu dhabihu.' 9Kazi iwe nzito zaidi kwa watu, ili waendelee kuifanya wasiyasikilize maneno ya uongo."
10Wasimamizi wa watumwa na wanyapara wakatoka wakawaambia watu, "Farao asema hivi: 'Sitawapa majani tena.' 11Nendeni mkajitafutie majani yenu wenyewe popote mtakapoyapata—lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.'" 12Basi watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri kukusanya mabua badala ya majani. 13Wasimamizi wa watumwa wakawahimiza wakisema, "Malizeni kazi yenu ya kila siku, kama vile mlipokuwa na majani." 14Wanyapara wa Waisraeli, ambao wasimamizi wa watumwa wa Farao walikuwa wamewaweka juu yao, wakapigwa na kuulizwa, "Kwa nini hamkutimiza kiasi chenu cha matofali jana na leo, kama zamani?"
15Ndipo wanyapara wa Waisraeli wakaja wakamlilia Farao, "Kwa nini unawatendea watumishi wako hivi? 16Watumishi wako hawapewi majani, lakini wanatuambia, 'Tengenezeni matofali!' Tazama, watumishi wako wanapigwa, kumbe kosa ni la watu wako mwenyewe."
17Farao akasema, "Wavivu! Ninyi ni wavivu! Ndiyo maana mnasema, 'Turuhusu twende tukamtolee Mungu dhabihu.' 18Sasa nendeni, fanyeni kazi. Hamtapewa majani, lakini ni lazima mlete kiasi chenu kamili cha matofali."
19Wanyapara wa Waisraeli wakaona ya kuwa wako katika taabu walipoambiwa, "Msipunguze kiasi chenu cha matofali cha kila siku." 20Walipotoka kwa Farao, wakawakuta Musa na Haruni wamesimama kuwangojea, 21wakawaambia, "Baba yetu na awaangalie na kuwahukumu, kwa maana mmetufanya tunuke mbele ya Farao na maofisa wake, mkatia upanga mkononi mwao ili watuue."
22Ndipo Musa akarudi kwa Baba yetu akasema, "Baba yangu Mwenye Enzi, kwa nini umeleta taabu juu ya watu hawa? Kwa nini ulinituma kamwe?
23Tangu nilipokwenda kwa Farao kunena kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa, wala hujawaokoa watu wako hata kidogo."