Wayahudi Wawashinda Adui Zao
9 1Katika mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, siku ya kumi na tatu—amri na tangazo la mfalme yalipopaswa kutekelezwa, siku ambayo adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala—mambo yaligeuka: Wayahudi wakawatawala wale waliowachukia. 2Wayahudi wakakusanyika katika miji yao kotekote katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, ili kuwashambulia wale waliotaka kuwadhuru. Hakuna aliyeweza kusimama mbele yao, kwa maana hofu yao ilikuwa imewaangukia mataifa yote. 3Maofisa wote wa majimbo, na maliwali, na watawala, na wasimamizi wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa maana hofu ya Mordekai ilikuwa imewaangukia. 4Mordekai akawa mtu mwenye nguvu katika nyumba ya mfalme; sifa zake zikaenea katika kila jimbo, kwa maana Mordekai mwenyewe akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi. 5Wayahudi wakawapiga adui zao wote kwa upanga, wakiua na kuangamiza, wakiwatendea walivyopenda wale waliowachukia. 6Katika ngome ya Shushani Wayahudi wakaua na kuangamiza watu 500. 7Pia wakamwua Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha, 8na Poratha, na Adalia, na Aridatha, 9na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Vaizatha. 10Wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi, wakawaua—lakini hawakuchukua nyara.
11Siku hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani ikaletwa kwa mfalme. 12Mfalme akamwambia Malkia Esta, "Katika ngome ya Shushani Wayahudi wameua na kuangamiza watu 500 na wana kumi wa Hamani. Je, wamefanya nini katika majimbo mengine yote ya mfalme? Sasa ni ombi lako gani? Nawe utapewa. Ni haja gani zaidi unayoiomba? Nayo itatimizwa."
13Esta akasema, "Kama ikimpendeza mfalme, Wayahudi walioko Shushani na waruhusiwe kutenda tena kesho kulingana na amri ya leo, na wana kumi wa Hamani wanyongwe juu ya miti."
14Mfalme akaamuru itendeke hivyo. Tangazo likatolewa katika Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani. 15Wayahudi walioko Shushani wakakusanyika tena siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, wakaua watu 300 huko, lakini hawakuigusa nyara.
16Wayahudi wengine waliokuwa katika majimbo ya mfalme wakakusanyika ili kuyalinda maisha yao, wakapata raha kutoka kwa adui zao, wakawaua 75,000 waliowachukia, lakini hawakuigusa nyara. 17Jambo hili likatokea siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; siku ya kumi na nne wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
18Lakini Wayahudi walioko Shushani wakakusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, wakapumzika siku ya kumi na tano, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. 19Ndiyo sababu Wayahudi wa vijiji vilivyo wazi huisherehekea siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kwa furaha, na karamu, na sikukuu, na kupelekeana zawadi za vyakula.
Sikukuu ya Purimu Yaanzishwa
20Mordekai akaandika mambo haya, akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote ya Mfalme Ahasuero, walio karibu na walio mbali, 21ili kuwaamuru waisherehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari kila mwaka, 22kuwa ndizo siku ambazo Wayahudi walipumzika kutoka kwa adui zao, na mwezi ule uliogeuka kwao kutoka huzuni kuwa furaha, kutoka maombolezo kuwa sherehe. Akawaambia waziweke kuwa siku za karamu na furaha, wakipelekeana zawadi za vyakula na zawadi kwa maskini. 23Wayahudi wakayafanya kuwa desturi yale waliyokuwa wameanza kuyatenda, kama vile Mordekai alivyowaandikia. 24Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amewapangia maangamizi, na alikuwa amepiga pur—yaani kura—ili kuwaponda na kuwaangamiza. 25Lakini jambo hilo lilipofika mbele ya mfalme, aliamuru kwa barua kwamba mpango mbaya aliokuwa amewapangia Hamani Wayahudi urudi juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe wanyongwe juu ya miti.
26Kwa hiyo siku hizo zikaitwa Purimu, kwa jina la neno pur, kwa sababu ya maneno yote ya barua hii, na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowapata. 27Wayahudi wakajifunga wenyewe, na wazao wao, na wote waliojiunga nao, kuziweka siku hizi mbili kila mwaka kwa wakati wake ulioamriwa, bila kukosa, kama ilivyoandikwa. 28Kila kizazi, na kila jamaa, na kila jimbo, na kila mji vinazikumbuka na kuziweka siku hizi; siku hizi za Purimu hazitakoma kamwe miongoni mwa Wayahudi, wala kumbukumbu yake haitatoweka kwa wazao wao.
29Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, wakaandika kwa mamlaka yote wakiithibitisha barua hii ya pili ya Purimu. 30Barua zikapelekwa kwa Wayahudi wote katika majimbo 127 ya ufalme wa Ahasuero—maneno ya amani na kweli, 31kuzithibitisha siku hizi za Purimu kwa nyakati zake zilizowekwa, kama vile Mordekai Myahudi na Malkia Esta walivyowaamuru, na kama walivyojiamuru wenyewe na wazao wao, nyakati za kufunga na maombolezo. 32Amri ya Esta ikazithibitisha kanuni hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kitabu cha kumbukumbu.