Agano la Baba na Daudi
7 1Mfalme alipokuwa amekaa nyumbani mwake, na Baba yetu akiwa amempa raha kutokana na adui zake wote waliomzunguka, 2mfalme akamwambia Nathani nabii, "Tazama sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, lakini sanduku la Baba yetu linakaa katika hema."
3Nathani akamwambia mfalme, "Nenda, ufanye yote yaliyomo moyoni mwako, kwa maana Baba yetu yu pamoja nawe."
4Lakini usiku uleule neno la Baba yetu likamjia Nathani, kusema:
5"Nenda umwambie mtumishi wangu Daudi: Baba yako asema hivi: 'Je, wewe ndiwe utakayenijengea nyumba ya kukaa ndani yake? 6Sijakaa katika nyumba tangu siku ile nilipowatoa Israeli kutoka Misri mpaka leo, bali nimekuwa nikihama toka mahali hata mahali nikiwa na hema kwa maskani yangu.' 7Popote nilipohama pamoja na Israeli wote, je, nilinena neno lolote kwa kiongozi yeyote wa Israeli niliyemwamuru kuwachunga watu wangu, nikisema, 'Kwa nini hamkunijengea nyumba ya mierezi?' 8Basi sasa umwambie mtumishi wangu Daudi: Baba wa majeshi ya mbinguni asema hivi: 'Nilikutwaa kutoka malishoni, kutoka kuyafuata makundi ya kondoo, ili uwe mtawala juu ya watu wangu Israeli. 9Nami nilikuwa pamoja nawe kila mahali ulipokwenda, nami nimewakatilia mbali adui zako wote mbele yako. Nami nitalifanya jina lako kuwa kuu, kama jina la watu walio wakuu sana duniani. 10Nami nitawawekea watu wangu Israeli mahali, na kuwapanda humo ili wakae mahali pao wenyewe pasipo kufadhaishwa. Wala watu waovu hawatawaonea tena kama zamani, 11tangu siku ile nilipowaweka waamuzi juu ya watu wangu Israeli. Nami nitakupa raha kutokana na adui zako wote. Tena Baba yako anakuambia ya kwamba yeye mwenyewe atakujengea nyumba. 12Siku zako zitakapotimia, nawe utakapolala pamoja na baba zako, nitalisimamisha kizazi chako baada yako, kitakachotoka viungoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. 13Yeye ndiye atakayelijengea jina langu nyumba, nami nitakiimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. 14Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapotenda dhambi, nitamrudi kwa fimbo ya wanadamu, na kwa mapigo ya wana wa Adamu, 15lakini upendo wangu wa agano hautamwondoka, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa mbele yako. 16Nyumba yako na ufalme wako vitathibitika milele mbele yangu; kiti chako cha enzi kitaimarishwa milele.'"
17Sawasawa na maneno haya yote na maono haya yote, ndivyo Nathani alivyomweleza Daudi.
Daudi Anamshukuru Baba Yake
18Ndipo mfalme Daudi akaingia na kuketi mbele za Baba yetu, akasema: "Mimi ni nani, Ee Bwana Baba, na nyumba yangu ni nini, hata umenifikisha mpaka hapa? 19Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana Baba, hata umenena pia habari za nyumba ya mtumishi wako kwa wakati ujao wa mbali. Je, hii ndiyo desturi yako kwa wanadamu wote, Ee Bwana Baba? 20Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana wewe wamjua mtumishi wako, Ee Bwana Baba. 21Kwa ajili ya neno lako, na kwa kadiri ya moyo wako mwenyewe, umetenda ukuu huu wote, na kumjulisha mtumishi wako. 22Kwa hiyo wewe ni mkuu, Ee Bwana Baba. Kwa maana hapana aliye kama wewe, wala hapana Mungu ila wewe, sawasawa na yote tuliyoyasikia kwa masikio yetu wenyewe. 23Tena ni taifa gani lililo kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Baba yetu alikwenda kulikomboa liwe watu kwa nafsi yake, na kujifanyia jina, na kuwatendea ninyi mambo makuu ya kutisha—akiwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, uliowakomboa kwa nafsi yako kutoka Misri? 24Nawe uliwathibitisha watu wako Israeli wawe watu wako milele; nawe, Baba yetu, ukawa Baba yao.
25Na sasa, Baba yetu, lithibitishe milele neno ulilolinena katika habari za mtumishi wako na nyumba yake, ukafanye kama ulivyoahidi.' 26Na jina lako litakuzwa milele, na watu watasema, 'Baba wa majeshi ya mbinguni ndiye Mungu juu ya Israeli.' Na nyumba ya mtumishi wako Daudi itathibitika mbele yako. 27Kwa maana wewe, Baba wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, umemfunulia mtumishi wako, ukisema, 'Nitakujengea nyumba.' Kwa hiyo mtumishi wako amepata ujasiri wa kukuomba maombi haya.
28Na sasa, Ee Bwana Baba, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ni kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako jambo hili jema. 29Basi sasa, uridhie kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele mbele yako. Kwa maana wewe, Ee Bwana Baba, umenena hayo, na kwa baraka yako nyumba ya mtumishi wako itabarikiwa milele."