Wimbo wa Daudi wa Ukombozi
22 1Daudi alimwambia Baba yetu maneno ya wimbo huu wakati Baba yetu alipomwokoa kutoka mkononi mwa adui zake wote na kutoka mkononi mwa Sauli. 2Akasema: Baba yangu ndiye mwamba wangu, ngome yangu, mwokozi wangu. 3Baba yangu, mwamba wangu, ambaye kwake ninakimbilia, ngao yangu na nguvu ya wokovu wangu, boma langu na kimbilio langu, mwokozi wangu—wewe unaniokoa kutoka udhalimu. 4Ninamwita Baba yangu, anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu. 5Kwa maana mawimbi ya mauti yalinizunguka; mafuriko ya uharibifu yalinitisha. 6Kamba za kaburi zilinizonga; mitego ya mauti ilinikabili. 7Katika dhiki yangu nilimwita Baba yangu; nilimlilia Mungu wangu ili anisaidie. Kutoka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu, na kilio changu kilifika masikioni mwake. 8Ndipo dunia ikatetemeka na kutikisika; misingi ya mbingu ilitetemeka na kutikisika, kwa sababu alikuwa na hasira. 9Moshi ulipanda kutoka puani mwake, na moto uteketezao ukatoka kinywani mwake; makaa yaliyowaka yaliwaka kutoka kwake. 10Alizipasua mbingu na kushuka chini, na mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake. 11Alipanda juu ya kerubi na kuruka; aliruka juu juu ya mabawa ya upepo. 12Alifanya giza kuwa hema lake kumzunguka— mawingu meusi ya mvua ya angani. 13Kutoka mng'ao uliokuwa mbele yake yaliwaka makaa ya moto. 14Baba yangu alinguruma kutoka mbinguni; Aliye Juu Sana aliipaza sauti yake. 15Alizituma mishale yake na kuwatawanya adui zake, akatupa umeme na kuwakimbiza. 16Mifereji ya bahari ilionekana, misingi ya ulimwengu ilifunuliwa kwa kukemea kwa Baba yangu, kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake. 17Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa katika maji yenye kina kirefu. 18Aliniokoa kutoka kwa adui yangu mwenye nguvu, kutoka kwa watesi wangu waliokuwa na nguvu kunizidi. 19Walinikabili katika siku ya msiba wangu, lakini Baba yangu alikuwa tegemeo langu. 20Alinitoa nje mahali penye nafasi; aliniokoa kwa sababu alipendezwa nami. 21Baba yangu alinitendea sawasawa na haki yangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu alinilipa. 22Kwa maana nimezishika njia za Baba yangu; sikumwacha Mungu wangu kwa uovu. 23Hukumu zake zote ziko mbele yangu; sikuziacha amri zake. 24Nilikuwa mkamilifu mbele yake, nami nilijilinda nisiwe na hatia yangu. 25Kwa hiyo Baba yangu alinilipa sawasawa na haki yangu, sawasawa na usafi wangu mbele ya macho yake. 26Kwa mwaminifu unajionyesha kuwa mwaminifu; kwa mkamilifu unajionyesha kuwa mkamilifu. 27Kwa msafi unajionyesha kuwa msafi, lakini kwa mkaidi unajionyesha kuwa mwerevu. 28Unawaokoa watu walioteswa, lakini macho yako yako juu ya wenye kiburi, ili kuwashusha chini. 29Kwa maana wewe ndiwe taa yangu, Baba yangu; hulibadilisha giza langu kuwa nuru. 30Kwa msaada wako naweza kushambulia jeshi; pamoja na Baba yangu naweza kuruka ukuta. 31Kwa habari ya Baba yangu, njia yake ni kamilifu; neno la Baba yangu halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake. 32Kwa maana ni nani aliye Mungu ila Baba yetu? Na ni nani aliye mwamba isipokuwa Baba yetu? 33Baba yangu ni kimbilio langu lenye nguvu; huifanya njia yangu kuwa kamilifu. 34Huifanya miguu yangu kuwa kama miguu ya kulungu na kunisimamisha imara mahali pa juu. 35Huizoeza mikono yangu kwa vita, hata mikono yangu iweze kupinda upinde wa shaba. 36Umenipa ngao ya wokovu wako, na upole wako umenifanya kuwa mkuu. 37Unaipanua njia chini yangu, hata vifundo vya miguu yangu visiteleze. 38Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza; sikurudi nyuma hata walipomalizika. 39Niliwateketeza na kuwaponda hata wasiweze kuinuka; walianguka chini ya miguu yangu. 40Ulinivika nguvu kwa ajili ya vita; uliwafanya wapinzani wangu wainame chini yangu. 41Uliwafanya adui zangu wanigeuzie visogo katika kukimbia, nami niliwaangamiza wale walionichukia. 42Walitazama, lakini hakuna aliyekuwapo wa kuwaokoa— hata kwa Baba yangu, lakini hakuwajibu. 43Niliwasaga wawe laini kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama matope ya barabarani. 44Uliniokoa kutoka mabishano ya watu wangu; ulinihifadhi niwe kichwa cha mataifa; watu nisiowajua sasa wananitumikia. 45Wageni wananyenyekea mbele yangu; mara wasikiapo, wananitii. 46Wageni wanavunjika moyo; wanatoka wakitetemeka katika ngome zao. 47Baba yangu yu hai! Ahimidiwe Mwamba wangu! Atukuzwe Baba yangu, Mwamba wa wokovu wangu! 48Ni Baba yangu anipatiaye haki na kuwashusha mataifa chini yangu. 49Ananitoa kutoka kwa adui zangu. Ulininyanyua juu ya watesi wangu; uliniokoa kutoka kwa mtu mkatili. 50Kwa hiyo nitakusifu kati ya mataifa, Baba yangu; nitaliimbia jina lako sifa. 51Yeye humpa mfalme wake ushindi mkuu na humwonyesha upendo wa agano mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.