Yehoyakimu Anaasi Babeli
24 1Wakati wa Yehoyakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi; Yehoyakimu akamtumikia miaka mitatu, kisha akageuka na kumwasi. 2Ndipo Baba yetu akatuma majeshi ya washambuliaji wa Babeli, wa Aramu, wa Moabu, na wa Amoni juu yake; akawatuma juu ya Yuda ili kuiangamiza, kama vile Baba yetu alivyokuwa amesema kwa vinywa vya watumishi wake manabii. 3Jambo hili likawapata Yuda kwa amri ya Baba yetu, ili kuwaondoa mbele za uso wake kwa sababu ya dhambi za Manase—yote aliyoyafanya, 4na pia kwa sababu ya damu isiyo na hatia aliyoimwaga, kwa maana alikuwa ameijaza Yerusalemu damu isiyo na hatia ambayo Baba yetu asingeisamehe. 5Nayo matendo mengine ya Yehoyakimu, yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
6Basi Yehoyakimu akalala pamoja na baba zake, na Yehoyakini mwanawe akawa mfalme mahali pake.
7Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa maana mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa nchi yote ya mfalme wa Misri, kutoka Kijito cha Misri hadi Mto Frati.
8Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala, naye akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani, wa Yerusalemu. 9Akafanya yaliyo maovu machoni pa Baba yetu, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
Yerusalemu Yachukuliwa Utumwani
10Wakati huo, watumishi wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walipanda kwenda Yerusalemu, nao mji ukazingirwa. 11Naye Nebukadneza mfalme wa Babeli mwenyewe akaufikia mji wakati watumishi wake walipokuwa wakiuzingira. 12Yehoyakini mfalme wa Yuda akatoka kwenda kwa mfalme wa Babeli—yeye, na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wake, na maofisa wake wa nyumbani—naye mfalme wa Babeli akamchukua mateka, katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. 13Akachukua kutoka huko hazina zote za nyumba ya Baba yetu na za jumba la kifalme, akavikatakata vyombo vyote vya dhahabu alivyokuwa amevifanya Sulemani mfalme wa Israeli kwa ajili ya hekalu, kama vile Baba yetu alivyosema. 14Akawahamisha Yerusalemu yote: wakuu wote, na mashujaa wote hodari—mateka 10,000—na mafundi wote na wahunzi. Hakusalia mtu ye yote ila watu maskini kabisa wa nchi. 15Akamhamisha Yehoyakini kwenda Babeli, pamoja na mama wa mfalme, na wake zake, na maofisa wake, na watu wenye vyeo wa nchi, akiwachukua kutoka Yerusalemu hadi Babeli. 16Mfalme wa Babeli akawahamisha kwenda Babeli watu wote wa vita 7,000, na mafundi 1,000 na wahunzi, wote wenye nguvu, wanaofaa kwa vita. 17Mfalme wa Babeli akamfanya Matania mjomba wa Yehoyakini kuwa mfalme mahali pake, akalibadili jina lake kuwa Sedekia.
Sedekia Anatawala Yuda
18Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, wa Libna. 19Akafanya yaliyo maovu machoni pa Baba yetu, kama vile Yehoyakimu alivyokuwa amefanya. 20Kwa sababu ya hasira ya Baba yetu, mambo haya yote yakatukia katika Yerusalemu na Yuda, hata alipowatupa mbali na uso wake. Kisha Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.