Sulemani Ajenga na Kupanga Ufalme Wake
8 1Baada ya miaka ishirini, ambayo katika hiyo Sulemani alijenga nyumba ya Baba yetu na jumba lake mwenyewe, 2Sulemani akaijenga upya miji ile ambayo Huramu alikuwa amempa, na kuwaweka wana wa Israeli humo.
3Kisha Sulemani akaenda kupigana na Hamath-soba, akaishinda. 4Akajenga Tadmori jangwani, pamoja na miji yote ya ghala aliyoijenga katika Hamathi. 5Akaijenga tena Beth-horoni ya Juu na Beth-horoni ya Chini kuwa miji yenye ngome, yenye kuta, malango, na makomeo, 6na Baalathi, na miji yote ya akiba ya Sulemani, na miji ya magari yake na ya wapanda farasi wake, na yote aliyotamani kuyajenga katika Yerusalemu, na Lebanoni, na katika nchi yake yote.
7Walikuwako watu waliobaki kutoka kwa Wahiti, na Waamori, na Waperizi, na Wahivi, na Wayebusi, ambao hawakuwa wa Israeli. 8Wazao wao waliobaki katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuwaangamiza, Sulemani akawatoza kazi ya shokoa, kama walivyo hata leo. 9Lakini Sulemani hakumfanya mtu ye yote wa wana wa Israeli kuwa mtumwa kwa kazi yake; bali walikuwa wapiganaji, na maakida wa maafisa wake, na maakida wa magari yake na wapanda farasi wake. 10Hawa ndio waliokuwa maakida wakuu wa mfalme Sulemani: mia mbili na hamsini waliowasimamia watu.
11Sulemani akampandisha binti Farao kutoka Mji wa Daudi hata nyumba aliyokuwa amemjengea, akisema, "Mke wangu hataishi katika nyumba ya Daudi mfalme wa Israeli, kwa maana ni patakatifu kila mahali sanduku la Baba yetu lilipoingia."
12Ndipo Sulemani akamtolea Baba yetu sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu aliyoijenga mbele ya ukumbi, 13kila siku kama ilivyotakiwa, kwa amri ya Musa: siku za Sabato, na Miandamo ya Mwezi, na sikukuu tatu za mwaka—Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, na Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda.
14Kwa kufuata kanuni za Daudi baba yake, akaziweka zamu za makuhani kwa utumishi wao, na zamu za Walawi kusifu na kuhudumu mbele ya makuhani kama kila siku ilivyotaka, na zamu za mabawabu katika kila lango, kwa maana Daudi mtu wa Baba yetu alikuwa ameamuru hivyo. 15Wala hawakuiacha amri ya mfalme kwa makuhani na Walawi katika jambo lo lote, wala katika habari za hazina.
16Kazi yote ya Sulemani ikakamilika, tangu siku ile nyumba ya Baba yetu ilipowekewa msingi hata ilipomalizika; nyumba ya Baba yetu ikawa kamili.
17Ndipo Sulemani akaenda Esion-geberi na Elothi, penye pwani ya bahari katika nchi ya Edomu. 18Huramu akampelekea meli kwa mikono ya watumishi wake, pamoja na mabaharia waliojua bahari; wakasafiri pamoja na watumishi wa Sulemani mpaka Ofiri, wakatwaa kama tani kumi na saba za dhahabu, wakazileta kwa mfalme Sulemani.