Asa Amtafuta Baba na Kupata Raha
14 1Abiya akalala pamoja na baba zake; wakamzika katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme, nayo nchi ikawa na amani miaka kumi. 2Asa akatenda yaliyo mema na sawa mbele ya macho ya Baba yetu. 3Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu, akazivunja nguzo takatifu, na kuzikata nguzo za Ashera. 4Akawaamuru Yuda wamtafute Baba yetu, Mungu wa baba zao, na kuishika sheria na amri. 5Pia akayaondoa mahali pa juu na madhabahu za kufukizia uvumba katika miji yote ya Yuda, nao ufalme ukawa na amani chini yake. 6Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, kwa maana nchi ilikuwa na amani. Hakupigana vita miaka hiyo, kwa sababu Baba yetu alimpa raha. 7Akawaambia Yuda, "Na tuijenge miji hii na kuizungushia kuta, minara, malango, na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tulimtafuta Baba yetu; tulimtafuta, naye akatupa raha pande zote." Basi wakajenga na kufanikiwa.
8Asa alikuwa na jeshi la watu 300,000 kutoka Yuda wenye ngao kubwa na mikuki, na watu 280,000 kutoka Benyamini wenye ngao na pinde—wote mashujaa hodari.
9Zera Mkushi akatoka kupigana nao akiwa na askari milioni moja na magari 300 ya vita, akisonga mbele hata Maresha. 10Asa akatoka kupigana naye, wakapanga vita katika Bonde la Sefatha huko Maresha. 11Ndipo Asa akamlilia Baba yetu Mungu wake: "Baba, ni wewe tu uwezaye kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee Mungu wetu, kwa maana tunakutegemea wewe, na kwa jina lako tunakabiliana na kundi hili kubwa. Wewe ndiwe Mungu wetu; mtu wa kufa asikushinde."
12Basi Baba yetu akawapiga Wakushi mbele ya Asa na mbele ya Yuda, nao Wakushi wakakimbia. 13Asa na watu wake wakawafuatia hata Gerari, nao Wakushi wakaanguka hata hakusalia hata mmoja, kwa maana walivunjwavunjwa mbele ya Baba yetu na jeshi lake. Watu wa Yuda wakachukua nyara nyingi. 14Wakaipiga miji yote iliyokuwa kandokando ya Gerari, kwa maana hofu ya Baba yetu ilikuwa imewaangukia. Wakaiteka nyara miji yote, kwa kuwa nyara nyingi zilikuwamo ndani yake. 15Pia wakazishambulia hema za wachunga mifugo, wakachukua kondoo wengi na ngamia, kisha wakarudi Yerusalemu.