Solomoni Amtafuta Baba huko Gibeoni
1 1Solomoni mwana wa Daudi akaimarisha utawala wake juu ya ufalme wake; Baba yetu alikuwa pamoja naye, akamfanya kuwa mkuu sana.
2Solomoni akasema na Israeli wote—majemadari wa maelfu na wa mamia, waamuzi, na kila kiongozi katika Israeli, wakuu wa mbari za jamaa. 3Solomoni na kusanyiko lote wakaenda mahali pa juu huko Gibeoni, ambapo palikuwa na hema ya kukutania ya Baba yetu, ambayo Musa mtumishi wa Baba yetu aliifanya jangwani. 4Lakini Daudi alikuwa amelipandisha sanduku la Baba yetu kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali alipokuwa amepatengeneza, akalisimamishia hema huko Yerusalemu. 5Nayo madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, aliifanya ilikuwa hapo mbele ya maskani ya Baba yetu; hivyo Solomoni na kusanyiko wakamtafuta Baba yetu hapo. 6Solomoni akapanda kwenda kwenye madhabahu ya shaba mbele ya Baba yetu penye hema ya kukutania, akatoa juu yake sadaka 1,000 za kuteketezwa.
7Usiku ule Baba yetu akamtokea Solomoni, akamwambia, "Omba unachotaka nikupe."
8Solomoni akamwambia Baba yetu, "Ulimwonyesha upendo mkuu wa agano Daudi baba yangu, nawe ukanifanya mfalme mahali pake. 9Sasa, Baba yangu, ithibitishe ahadi yako kwa baba yangu Daudi, kwa maana umenifanya mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. 10Nipe hekima na maarifa sasa niwaongoze watu hawa, kwa maana ni nani awezaye kuwatawala watu wako hawa walio wengi?"
11Baba yetu akamwambia Solomoni, "Kwa sababu jambo hili lilikuwa moyoni mwako—hukuomba mali, utajiri, au heshima, wala uhai wa adui zako, wala maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa upate kuwatawala watu wangu, ambao nimekufanya mfalme juu yao, 12hekima na maarifa umepewa. Nami nitakupa pia mali, utajiri, na heshima, ambavyo hakuna mfalme aliyekuwako kabla yako aliyekuwa navyo, wala hakuna atakayekuwa navyo baada yako."
13Basi Solomoni akatoka mahali pa juu pa Gibeoni, kutoka mbele ya hema ya kukutania, akaenda Yerusalemu; naye akatawala juu ya Israeli.
14Solomoni akakusanya magari ya vita na wapanda farasi; alikuwa na magari 1,400 na wapanda farasi 12,000, ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita na pamoja na mfalme huko Yerusalemu. 15Huko Yerusalemu mfalme akaifanya fedha na dhahabu kuwa nyingi kama mawe, na mierezi kuwa mingi kama mikuyu ya tambarare za chini ya vilima. 16Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na Kue; wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue kwa bei ya sokoni. a a v16 Kue lilikuwa eneo katika sehemu ambayo sasa ni kusini mwa Uturuki, lililothaminiwa katika ulimwengu wa kale kwa ajili ya farasi wake. 17Waliagiza gari la vita kutoka Misri kwa kiasi cha ratili kumi na tano za fedha, na farasi kwa kiasi cha ratili nne; kupitia kwao waliyauza haya kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Aramu.